Bwana Yesu asifiwe, kuanzia tarehe 1/1/2017 tutakuwa tukihamia katika website yetu iitwayo www.egospeltz.org

ARCHIEVE 1


UNAHITAJI WAZO JIPYA KUTOKA KWA MUNGU ILI UTOKE MAHALI ULIPO
Mwaka 2010 nilikwenda Mbeya kwa mapumziko ya likizo na familia yangu. Wakati huo kuna mambo kadhaa nilikuwa nayapitia ambayo yalikuwa yakinipa shida rohoni mwangu na nilitamani kuvuka kutoka hapo na kwenda hatua nyingine bora ya mafanikio. Hivyo nikadumu kumwomba Mungu anifungulie mlango na kunipeleka hatua nyingine. Katika kuendelea kuomba na kutafakari neno la Mungu ndipo nikasikia sauti ndani yangu ikisema ‘usipokuwa na wazo jipya huwezi kutoka mahali ulipo’. Ingawa neno hili lilikuwa jibu kwangu, ilinichukua muda mrefu kuelewa Mungu alimaanisha nini. Ndipo nikaendelea kuomba na kujifunza kutoka kwenye Biblia kuhusu jambo hili pamoja na kusoma vitabu kadha wa kadha. Kwa sababu hii nimeona ni vema nikushirikishe uzoefu wangu ambao nina amini na wewe utakusaidia pia.

Nilijifunza kwamba maamuzi ya mtu ni matokeo ya mawazo yake, na matendo ya mtu ni matokeo ya mawazo anayowaza jumlisha maamuzi anayotekeleza. Naam hii ina maana kwamba, kumbe wazo au mawazo yana nafasi kubwa sana katika kubadilisha maisha ya mtu kwa kumtoa hatua moja na kumpeleka hatua nyingine. Ni muhimu ujifunze kutafuta mawazo mapya ili kubadili maisha yako kuwa bora zaidi ukikumbuka kwamba Mungu anakuwazia mawazo ya amani daima (Yeremia 29:11).

Wazo ni nini?

Wazo ni mpango, lengo, pendekezo, dhana au picha ambayo Mungu, Shetani huweka au kupanda ndani ya mtu (moyoni) ili mtu alifanyie kazi na hivyo kufanikisha makusudi ya ufalme wake hapa duniani. Kama umesoma mfululizo wa masomo yangu juu ya vita vya kiroho ambayo niliandika siku za nyuma nimeeleza kwa upana sana juu ya namna Mungu, Shetani kila mmoja anavyotumia mawazo kuhakikisha makusudi yao yanafanikiwa hapa duniani, na hivyo kufanya vita vya kiroho kuwa vita ya mawazo.

Ukisoma Biblia utagundua kuna vyanzo vitatu vya mawazo navyo ni; a) kuna mawazo kutoka kwa Mungu (Yeremia 29:11), b) kuna mawazo kutoka kwa Shetani (2 Wakorinto 4:4) na c) kuna mawazo kutoka kwa mtu au watu (Isaya 65:2). Mwanadamu anapita katika hatua mbalimbali za maisha kama misiba, njaa, magonjwa, dhiki, kushindwa kufikia malengo, hali ngumu kiuchumi nk. Ni furaha sana kwenye ufalme wa giza kuona watoto wa Mungu wanaishi maisha ambayo Mungu hakuwapangia, namaanisha maisha ambayo mtu anaishi nje ya mawazo ya Mungu juu yake. Naam hii ndio kazi anayokazana kuifanya Shetani ya kuwafarakanisha watu na Mungu wao.

Zifuatazo ni hatua zitakazokusaidia kupata wazo jipya la kukutoa katika hali ya maisha ambayo wewe binafsi huridhiki nayo na kukupeleka kwenye eneo bora zaidi kimafanikio;

1. Ni muhimu kujua mahali ulipo sasa
Hili ndio jambo la msingi kabisa la kuanza nalo ili kupata wazo jipya. Kimsingi unatakiwa kujua hali yako ya sasa ya kiroho, kifamilia, kihuduma, kiuchumi, kibiashara, kifamilia, kimahusiano nk. ikoje au ni ya namna gani? Je unaridhika nayo au la? kwa nini huridhiki nayo nk. Hali yako ya sasa ni matokeo ya kuwaza kwako juu ya hilo eneo. Kwa hiyo licha ya kujua mahali ulipo jiulize ni wazo au mawazo gani ambayo yalikufikisha mahali ulipo. Kwa lugha nyingine jiulize kwa nini upo ulivyo?Yawezekana upo ulipo kwa sababu kuna mawazo fulani yaliingia moyoni mwako nawe ukayatafakari na kisha kuyafanyia kazi na ndio maana umefika mahali ulipo. Kumbuka maisha ya mtu ni matokeo ya mawazo na maamuzi anayotekeleza maishani mwake. Mfano; kutokutoa zaka na sadaka kwa uaminifu (Malaki 3:7-10), kukosa uaminifu, uongo au kumpa ibilisi nafasi nk ni vyanzo vya laana kwenye maisha ya mtu.



 2.  Fahamu mahali unapotakiwa au unapotaka kwenda.
Kama huridhiki na hali yako ya sasa ya maisha, hii ina maanisha kuna hali nyingine bora zaidi ambayo unatamani kuifikia. Kwa sababu hii unahitaji kuanza kufikiri au kuwaza ni wapi unataka kwenda/kufika kwa maana ya mafanikio, ni hatua gani ya mafanikio kiroho, kihuduma, kifamilia, kibiashara nk unataka kuifikia maishani mwako? Naam unatakiwa kutoridhika na mazingira uliyonayo ili kuweka kiu ya wazo la kukutoa mahali ulipo.

3. Tumia Biblia kama msingi wa kupata mawazo/wazo jipya
Biblia inasema katika Yeremia 29:11 ‘Maana nayajua mawazo ninayowawazia ninyi, asema BWANA, ni mawazo ya amani wala si ya mabaya, kuwapa ninyi tumaini siku zenu za mwisho’. Ni muhimu ukafahamu kwamba neno la Mungu ni jumla ya mawazo ya Mungu juu ya namna gani watoto wake wanapaswa kuishi ili kufanikisha maisha yao na kusudi lake hapa duaniani.Biblia imejaa mawazo mapya toka kwa Mungu (Mithali 16:20, Joshua 1:8, Mithali 20:5). Naam bila kuwa na wazo jipya huwezi kutoka mahali ulipo. Soma kwa kulitafakari neno la Mungu, ndivyo utakavyojua kwa hakika Mungu anakuwazia mawazo ya amani kwenye kila eneo la maisha yako kuliko ulivyokuwa unafikiri.

4. Jifunze kuwa na muda wa kuwaza
Hili ni jambo ambalo Shetani amefanikiwa kuwafunga watu wengi sana wasiliweke kwenye matendo. Mungu amemuumba mtu kwa namna ambayo kama mtu atakuwa na nidhamu ya kutenga muda kwa ajili ya kuwaza kile ambacho Mungu anaweka kwenye moyo wa mtu, basi maisha ya mwanadamu yange kuwa bora sana licha ya changamoto nyingi zinazomkabili. Ni muhimu sana kwako kama mtoto wa Mungu kuwa na muda wa KUWAZA. Tafadhali nieleweke vema sijasema muda wa kuomba au kusoma neno, bali muda wa KUWAZA/KUFIKIRI kile Mungu anataka ukifanye hapa duniani kupitia mawazo anayotelemsha moyoni mwako. Jijengee nidhamu hii utaona mabadiliko makubwa sana kwenye kila eneo la maisha yako, anza hata kuwa na dakika kumi na tano, nusu saa, saa moja nk. (Zaburi1:1-2)

5. Jifunze kufikiri kwa nyakati au ki-muda.
(1 Nyakati 12:32, Kumbukumbu 32:29, Luka 19:41-45). Biblia iko wazi katika kitabu cha Mhubiri 3:1 ikisema ‘Kwa kila jambo kuna majira yake, na wakati wa kila kusudi chini ya mbingu’. Hii ina maana kila kusudi ambalo mwanadamu amepewa limefungwa kwenye muda na hivyo mwanadamu lazima ajifunze kushirikiana na kuukomboa muda/wakati (Waefeso 5:16) ili maisha yake binafsi yawe na mafanikio lakini pia kusudi la BWANA.Hivyo tunajifunza kwamba kwa mujibu wa (Mhubiri 3: 1) ili mwanadamu aweze kushirikiana vema na muda, ni lazima ndani yake ajifunze kufikiri ki- muda (thinking in terms of time). Naam kila wazo au kusudi linalokuja moyoni mwake toka kwa Mungu, basi mosi atafute kujua muda wa hilo wazo kutimia ni lini , na pili ajifunze kuweka muda kwa kila mikakati au mipango ambayo anaiweka kwa ajili ya kutekeleza wazo husika. Mfano: Ni imani yangu kwamba Nuhu alipoambiwa tengeneza Safina, ndani yake alipiga mahesbu ya muda unaohitajika kwa ujumla na hivyo kila hatua ya ujenzi akaiwekea muda mpka Safina ilipokamilika.


Naam unahitaji wazo jipya kutoka kwa Mungu ili kutoka mahali ulipo kiroho, kiuchumi, kibiashara nk. Tafuta wazo jipya toka kwa Mungu, naam Kwa mapato yako yote jipatie ufahamu (Mithali 4:7)



YOU HAVE TO BE A PROBLEM SOLVER AND NOT A PROBLEM CREATOR

Unapozaliwa kuja ulimwenguni kutokana na Yer 1:5 unakuja kwa mpango maalumu wa Mungu. Hii ndio sababu ya wewe kuwa "Problem solver na sio problem creator" .Ndio maana duniani hatuwezi kufanana kwa kuwa kila mtu aliletwa na ya kwake ila tunasaidiana tu ili kutimiza yalio mbele yetu.

Yusufu alijua kuwa yeye ni problem solver ndio maana haikumsumbua ndugu zake kumkataa Mw 37:11 wala Mke wa Potifa Mw 39:7-12. Maana alijua kuwa kama angefanya jambo lolote la kinyume lingesababisha awe problem creator. Hivyo kwenda kwake jela kulimfanya ajue kuwa ndio njia sahihi ambayo ingemfanya awe problem solver. Tunaona  katika Mw 41:14-16, 28-36 Yusufu anaitwa na Farao kutoa ufafanuzi wa njozi na alikwenda kifua mbele maana alijua ndio Bwana alilomwitia kwa maana nyingine waliingia kwenye fani yake.

Pia tunaona wako problem solvers wengine ambao wamejitokeza kwenye biblia. Wachache wao ni Ibrahim, Daudi na Yesu. Ibrahim alipopewa habari na malaika juu ya kuchomwa kwa Sodoma alianza kuiombea na sio kutangaza alichoambiwa hii ni tofauti kwa watu wengi ambao pengine wangetangaza kwa watu na kufurahi kama pengine watu wa Sodoma wangekuwa adui zao.

Hata Daudi naye alikuwa ni mfano wa problem solver. Yeye wakati anachunga kondoo alihakikisha simba na dubu hawafikii kondoo. Licha ya hilo baada ya kuwatembelea kaka zake vitani na kugundua wote wameshindwa aliona ni wakati wa yeye kusaidia 1Sam 17:34-36.

Yesu ndie mfano asiye na kifani kwani alikwenda mbali zaidi kutatua matatizo ya vizazi vijavyo. Unaposoma Isa 53:5 alitatua tatizo la magongwa, Mk 16:17 amempa kila nguvu juu ya mapepo, 2 Kor 8:9 ametufanya kuwa matajiri na 1Yoh 5:4 ameufanya ushindi kuwa asili yetu. Hivyo utaona namna ambavyo Yesu alisimama kama "Problem Solver".

Chukua hatua…………………………………………………………………………………………………………………………………..!

Barikiwa sana

Na Henry Nicholaus.



KUTOKUTOA ZAKA NA DHABIHU NI KUMWIBIA MUNGU

Mtu aliye mkristo asipotoa zaka na dhabihu anaitwa mwizi. Kuna wakristo ambao ni wezi lakini wao hawajui yakuwa ni wezi. Wamemwibia Mungu zaka na dhabihu. Mungu anasema hivi:  “Je! mwanadamu atamwibia Mungu? Lakini ninyi mnaniibia mimi. Lakini ninyi mwasema, tumekuibia kwa namna gani? Mmeniibia ZAKA na DHABIHU” (Malaki 3:8)

 Kati ya amri tulizopewa na Mungu ni kwamba tusiibe. Kuiba ni dhambi. Na dhambi ina adhabu yake. Popote palipo na dhambi, laana hutokeza. Kwa wale wanaomwibia Mungu kwa kutokutoa zaka na dhabihu, wamefunikwa na laana. Ndiyo maana Mungu alisema hivi: “….. Mmeniibia Zaka na Dhabihu. Ninyi mmelaaniwa kwa laana; maana mnaniibia mimi, naam, taifa hili lote (Malaki 3:8b, 9). Laana maana yake ni kutokufanikiwa, kutofaulu, kutokustawi, kukosa furaha, kukosa amani, na kukosa mwelekeo sahihi. Ni wazi kuwa wakristo wengi hawana furaha, hawana amani na hawafanikiwi katika maisha yao ya kila siku, kwa sababu hawamtolei Mungu zaka na dhabihu. Unapokosa kumtolea Mungu ili ujenzi wa nyumba yake – kanisa uendelee, (Hagai 1:6) anatuambia Mungu anasema hivi; “Mmepanda mbegu nyingi mkavuna kidogo; mnakula lakini hamshibi; mnakunywa lakini hamkujazwa na vinywaji; mnajivika nguo lakini hapana aonaye moto; na yeye apataye mshahara apata mshahara ili kuutia katika mfuko uliotoboka-toboka”.

 Zaka ni kitu gani? Zaka ni fungu la kumi la pato lako. Hebu isome na kuitafakari mistari ifuatayo; “Tena zaka yote ya nchi, kama ni mbegu ya nchi, au kama ni matunda ya nchi, ni ya Bwana, ni takatifu kwa Bwana ….Tena zaka yote ya ng’ombe, au ya kondoo, kila apitaye chini ya fimbo; SEHEMU YA KUMI watakuwa ni watakatifu kwa Bwana” (Mambo ya Walawi 27:30 –32). “…Toa fungu la kumi lote la maongeo yako ya mwaka huo, uliweke ndani ya malango yako; na Mlawi kwa kuwa hana fungu wala urithi pamoja nawe, na mgeni, na yatima, na mjane aliyefiliwa na mumewe, walio ndani ya malango yako, na waje wale na kushiba; ili kwamba Bwana, Mungu wako, akubarikie katika kazi yote ya mkono wako uifanyayo”(Kumbukumbu la Torati 14:28-29). Zaka ni fungu la kumi la pato toka mshahara wako ofisini, shambani au kwenye mifugo. Tena zaka hii ni ya Bwana na ni Takatifu. Mtu asipoitoa zaka hii anamwibia Mungu. Zaka si yako hustahili kukaa nayo wala kuitumia nje ya utaratibu wa Mungu. Lakini Malaki 3:10a anasema; “Leteni zaka KAMILI ….” Maana yake nini maneno haya? Maana yake ni hii; ikiwa kwa mfano mshahara wako kwa mwezi ni shilingi 2,000/= ( kabla ya makato) – fungu la kumi au zaka unayotakiwa kutoa ni shilingi 200/= ambayo ndiyo zaka kamili ya mshahara wako. Ukileta pungufu yake hiyo si zaka kamili. Tena kwa mfano umevuna magunia 10 ya mahindi toka shambani mwako – zaka kamili unayotakiwa kutoa ni gunia moja bila kupungua. Kumbuka mzaliwa wa kwanza wa mifugo yako ni wa Bwana.

 Unaweza ukasema habari za kutoa zaka ni za agano la kale na siyo za agano jipya. Waebrania 7:5-10 inatuambia wazi ya kuwa Ibrahimu alitoa fungu la kumi. Kama Ibrahimu alitoa sehemu ya kumi, Je! si zaidi sana kwetu sisi tulio uzao wake kwa imani ndani yake Kristo? Maana imeandikwa hivi; “Na kama ninyi ni wa Kristo, basi, mmekuwa uzao wa Ibrahimu na warithi sawasawa na ahadi” (Wagalitia 3:29). Soma pia Wagalitia 3:13,14).

 Dhabihu ni kitu gani? Dhabihu ni matoleo yanayotolewa baada ya kutoa sehemu ya kumi ya pato lako. Kwa mfano, kama mshahara wako kwa mwezi ni shilingi 2,000/=, basi sehemu ya kumi (zaka) ni shilingi 200/=. Kiasi cho chote utakachotoa ju ya shilingi 200/= ndiyo matoleo yako. Kwa mfano ukitoa shilingi 210/= toka kwenye mshahara wako wa shilingi 2000/=, Basi, shilingi 200/= ni zaka; na shilingi 10/= ni dhabihu au matoleo au sadaka ya kawaida. Kiasi utakachotoa katika dhabihu/matoleo, ndicho kitakachokuwa kipimo kitakachoweka kiwango chako cha kupokea. Imeandikwa hivi: “Lakini nasema neno hili, APANDAYE HABA ATAVUNA HABA; APANDAYE KWA UKARIMU ATAVUNA KWA UKARIMU. Kila mtu na atende kama alivyokusudia moyoni mwake, si kwa huzuni, wala si kwa lazima; maana Mungu humpenda yeye atoaye kwa moyo wa ukunjufu. Na Mungu aweza kuwajaza kila neema kwa wingi, ili ninyi, MKIWA NA RIZIKI ZA KILA NAMNA SIKU ZOTE,mpate kuzidi sana katika kila tendo jema ;kama ilivyoandikwa, Ametapanya, amewapa maskini, haki yake yakaa milele. Na yeye ampaye mbegu mwenye kupanda, na mkate uwe chakula, atawapa mbegu za kupanda na kuzizidisha, naye ATAYAONGEZA MAZAO YA HAKI YENU, MKITAJIRISHWA KATIKA VITU VYOTE MPATE KUWA NA UKARIMU WOTE; umpatiao Mungu shukrani kwa kazi yetu. Maana utumishi wa huduma hii HAUWATIMIZII WATAKATIFU RIZIKI WALIZOPUNGUKIWA TU, Bali huzidi sana kuwa na faida kwa shukrani nyingi apewazo Mungu; kwa kuwa mkijaribiwa kwa utumishi huo, WANAMTUKUZA MUNGU kwa ajili ya utii wenu katika kuikiri Injili ya Kristo, na kwa ajili ya ukarimu wenu mliowashirikisha wao na watu wote” (2Wakorintho 9:6-13)

Soma tena mistari hiyo hapo juu, lakini sasa tafakari zaidi maneno niliyoyaandika kwa herufi kubwa. Utaona kuwa usipokuwa mwaminifu katika utoaji, wewe mwenyewe unakosa kufanikiwa, na pia unamkosesha Mungu shukrani na utukufu ambao angepata kwa utoaji wako.

 Zaka na dhabihu zitolewe wapi? Hili jambo linahitaji uongozi wa Roho Mtakatifu, ili upate ufahamu Mungu anataka upeleke wapi zaka na matoleo uliyo nayo. Hili ni muhimu kwa kuwa Biblia inazungumza juu ya kupeleka kanisani (Malaki 3:10-11), kwa watakatifu (2Wakorintho 9:12), kwa maskini (2Wakorintho 9:8-9), kwa watumishi wa Mungu (1Wafalme 17:10-24; 1Wakorintho 9:7-14); kwa wajane, - na kadhalika. Muombe Mungu akuongoze mahali pa kupeleka. Amani ya Kristo na iamue moyoni mwako. Baraka Tele! Kuna baraka tele za mafanikio kwa mkristo aliye mwaminifu katika kumtolea Mungu zaka na matoleo. Katika Malaki 3:10 imeandikwa hivi; “Leteni zaka kamili ghalani, ili kiwemo chakula katika nyumba yangu, mkanijaribu kwa njia hiyo (YA UTOAJI) asema Bwana wa Majeshi; mjue kama sitawafungulia madirisha ya mbinguni, na KUWAMWAGIENI BARAKA, HATA ISIWEPO NAFASI YA KUTOSHA AU LA” .

 Je! umewahi kukutana na mkristo ambaye anashuhudia kuwa Mungu amempa baraka nyingi hata HANA MAHALI PA KUZIWEKA? Ni wazi kuwa ahadi hii haijatimia kwa kuwa hatujawa watendaji na Neno kikamilifu katika utoaji. Soma mistari hii hapa chini uone baraka zingine zinazotokana na utoaji; “Azaria Kuhani Mkuu, wa nyumba ya Sadoki, akamjibu, akasema, Tangu watu walipoanza kuleta matoleo nyumbani kwa Bwana, tumekula na KUSHIBA NA KUSAZA TELE; kwa kuwa Bwana amewabariki watu wake; na kilichosalia ndiyo akiba hii kubwa. Ndiko Hezekia akaamuru kutengeneza vyumba nyumbani mwa Bwana; wakavitengeneza. Wakayaingiza MATOLEO na ZAKA na vitu vilivyowekwa wakfu, kwa uaminifu ….” (2Mambo ya Nyakati 31:10-12). Kwa nini wakristo wengine wanapungukiwa vyakula, wakati tuna nafasi ya kumruhusu Mungu kutubariki kwa vyakula tele?

Mpe Mungu nafasi ya kukubariki kwa kumtolea zaka na matoleo! Anza Sasa! Nakushauri ya kuwa kama ulikuwa hutoi sehemu ya kumi au zaka pamoja na matoleo ya kutosha – anza sasa. Jambo la kwanza, kumbuka kutubu kwa Mungu katika Jina la Yesu Kristo kwa kuwa ulimwibia zaka na dhabihu kwa kutokumtolea. Halafu mwombe Mungu akuwezeshe kusimama katika uaminifu wa kumtolea zaka na dhabihu ili apate nafasi ya kukubariki zaidi kama tulivyoona, na kama alivyoahidi.

Na Mwl Christopher Mwakasege.



ACHANA KUCHEZA NA NEEMA YA MUNGU MAANA WATU WA KALE WALIITAFUTA KWA JASHO.

Tukisoma Luka 19:1-10 tunaona kuwa kulikuwa na mtu mmoja jina lake Zakayo huyu alikuwa mtoza ushuru ambaye alikuwa na shauku kubwa ya kukutana na Yesu hivyo kwa sababu ya ufupi aliokuwa nao akaazimia apande juu ya mkuyu ili apate kumwona Yesu.

Katika kipindi cha maisha tulionayo tumepewa neema kubwa ya kusikia neno la Mungu. Utaona hilo kwa kuwa kuna vipindi vya redio, televisheni na hata magazetini kumekuwa na machapisho ya neno la Mungu. Mikutano ya hadhara, makongamano na semina za neno la Mungu zimeshamiri. Hii ni kimo cha kuonyesha neema ya Mungu imefunuliwa ili tumfahamu yeye kwa zaidi.

Sasa katika kipindi cha nyuma tunaona Zakayo alitumia nguvu mno ili apate kumwona Yesu hata kuweza kukubali aibu ya kupanda juu ya mti kusudi tu apate kuweza kukutana na Yesu. Leo hii ukienda mtandaoni Yesu yupo, mtaani yupo, makazini yupo, mashuleni yupo na makanisani yupo hivyo utaona kuna neema ambayo mpendwa umefunuliwa ili umjue Mungu.

Ndugu mpendwa kumia fursa hii kwa mapana maana hujui kama neema yako inakoma lini neema ya Mungu ni moja lakini haifanani katikati ya watu maana kila mtu hupewa kwa kadiri ya kujisogeza kwake mbele za Bwana. Ukiacha hii neema ikupite utajilaumu baadae na ushindwe kubadili uhalisia.

Mhu 12:1 inasema "Mkumbuke Muumba wako siku za ujana wako, Kabla hazijaja siku mbaya, Wala haijakaribia miaka utakayosema, Mimi sina furaha katika hiyo."Mhubiri anaeleza kwa nini tutumie neema hii vizuri na nini hasara zake. Hivyo wewe kijana unayenifuatia kupitia E Gospel chukua hatua madhubuti kuanza kuitendea kazi jambo hili.

Nimatumaini yangu hakuna wa kumlaumu pindi ile neema ya Mungu iliofunuliwa itakapofungwa kwako kwa maana jambo hili mwimbaji wa nyimbo za injili Bonny Mwaitege alisema uko wakati neema itatoweka tutamani kuokoka haitawezekana. Chukua hatua sasa maana wakati uliokubalika ni sasa na sio baadae.

Na Henry Nicholaus

Barikiwa Sana


 
HUU NI WAKATI WA KUTEMBEA KWENYE VIWANGO VYA USHINDI
Siku ulio zaliwa mara ya pili ndio siku ambayo ulizaliwa katika maishi ya ushindi yasiyo kuwa mwisho. Kifo cha Yesu pale msalabani kilikufanya wewe uwe pamoja na Mungu na kuunganishwa nae. Unaposoma Yn 15 unaona Yesu anazungumza kuwa yeye ni mzabibu na sisi tu matawi hili ni kudhihirisha hayo.
Watu wengi wanaamini kuwa maisha yamejaa matatizo ni kwa sababu hawajafahamishwa uhalisia wa Injili ya Yesu mwenyewe. Wewe kama mtoto wa Mungu umeitwa kuishi maishi ya ushindi kila siku katika kila linalokujia mbele zako. Haya ndio maisha halisi ya waaminio.
Ushindi kwa waaminio ni haki yao ya kuzaliwa, ndio maana Mungu ametuinua na kutuketisha pamoja na Yesu mbinguni Efe 2:6. Hivyo Mungu ametuketisha juu sana kuliko ufalme wote, na mamlaka, na nguvu, na usultani, na kila jina litajwalo wala sio wa ulimwenguni humu tu, bali katika ule ujao Efe 2:21 Hivyo Mungu amekuketisha mbali na sio karibu.
Shetani na falme za giza na kila nguvu ya kinyume umewekwa juu yake mno. Hivyo umekwisha kuvishinda vitu hivi, hivyo tembea katika nuru ya ushindi hivyo iwe mtazamo wako kila wakati kuwa wewe haushindiki maana ndio uhalisia wako.
Hivi nataka uendelee kujua kuwa huu ni wakati muafaka wa wewe kutembea katika ushindi juu ya dhambi, magonjwa, shetani, kifo na vikwazo mbalimbali katika maisha. Ilimradi Mungu anahusika katika ulimwengu huu hakuna cha kukushinda. "… mmewashinda kwa sababu aliye ndani yenu ni mkuu kuliko aliye katika dunia".
Huu ni wakati wako mpendwa wewe unayefuatana nami katika ujumbe huu wa kudhihirisha ushindi wako uliopewa na Yesu
Barikiwa
Na Henry Nicholaus


 USHUHUDA NI NGUVU

Tunaposoma Ufu 12:11 inasema "Nao wakamshinda kwa damu ya Mwana Kondoo, na kwa neno la ushuhuda wao; ambao hawakupenda maisha yao hata kufa". Wakristo wengi bado hatujajua kuwa ushuhuda ni nguvu ya kumshinda ibilisi.

Unapoingia mahali popote pa ugeni ni vyema ukashuhudia ili kujitambulisha katika hilo eneo maana unapojitambulisha mapepo wanajua wewe ni nani na kama unasogeleka au la. Unaposhuhudia wanatambua profile yako, hivyo kuwafanya nao washuhudiane wenyewe kuwa mtu huyu haingiliki. Ndio maana neno lasema kuwa Nao wakamshinda kwa damu ya Mwana Kondoo, na kwa neno la ushuhuda.

Tunaona ushuhuda umekuwa sababu tosha ya kuwafanya washinde.Mapepo hawapendi matatizo  ndio maana watatangaaziana kuwa huyu si wa kumwendea. Lakini kama ukijiendea bila wao kujua profile yako lazima watakujaribu. Technique ni muhimu katika maisha na sio nguvu.

Tunaweza kushuhudia vile ambavyo Mungu amefanya kwenye maisha yako kama sivyo sema vile ambavyo umemwona  Mungu akifamya kazi yake kwa watu wengine na hata kwenye biblia. Kushuhudia sio kujisifu kama wengine wanavyodhani bali ni njia ya kumshinda ibilisi. Sababu hii ndio aitumiayo ibilisi kuweza kuwanyong'onyeza wengi.

Ondoa aibu  anza kushuhudia kwa kasi ya ajabu ili umshinde ibilisi.



BILA UNYENYEKEVU TUTASHUSHWA UTUKUFU
Unyenyekevu ni ile hali ya kujishusha kwa kujiona kuwa wewe si kitu mbele ya watu wengine, mamlaka au kitu chochote. Utukufu ni hali uwepo wa juu alionao mtu, kitu au mamlaka
Katika Mdo 12:20-23 Herode aliketi kwenye kiti chake cha enzi hata akatoa hotuba. Kwa uzuri wa hotuba yake watu wakampigia makelele wakisema, "Ni sauti ya Mungu na si mwanadamu" kwa kuwa Herode alipokuwa akiyasikia hayo hakuona nafasi ya kumtunguza Mungu maana haikuwa kwa uwezo  wake. Hivyo basi akapigwa na malaika akaliwa na chango akafa.
Somo hili linatufundisha habari ya unyenyekevu. Mara nyingi watumishi wengi huanguka kwa sababu hiki kitu hawakijui. Unajua uweza wa Mungu ulio ndani yetu unafanya mambo makubwa kuliko hata yale tuyaombayo Efe 3:20. Hivyo basi bila hata kuwa makini tunaweza kujikuta mtu anaona ni uweza wake unaofanya hivyo. Na matokeo yake kuwa ni mwisho wa huduma yake. Maana ni wale wachache ambao humudu kuomba toba na kurejea.
Sisi kama wanadamu chochote tunachokifanya basi tambua ya kuwa tumepewa kibali na Bwana na ndio maana twaweza kufanya. Kwa hiyo tusifikiri katika uweza wetu maana ni mdogo mno. Isa 55:9 inatuambia mawazo ya Mungu ni mawazo yalio juu sana kuliko yale ya kwetu. Kwa hiyo mpaka hapa utaona kuwa mwanadamu uwezo wake una mipaka. Hivyo anapopewa uweza zaidi ni muhimu akatambua kuwa ili neema ile iendelee kumkalia ni lazima anyenyekee.
Unapoona Mfano mtu wa Mungu Tb Joshua anafanya makubwa hii ina maana kuwa yeye ameelewa kwa viwango vya juu sana somo la unyenyekevu. Huwezi kumwona akijivuna kuwa ni yeye afanyaye mambo anayofanya. Bali anajua uwezo ulio ndani yake ndio uliompa kibali cha kuweza kufanya mambo yaliyo makubwa.
Ndugu mpendwa mambo makubwa hayakuumbiwa watu fulani. Maana inawezekana ikawa ni mtazamo wako nataka utambue leo Mungu amempa kila mtu nafasi hiyo atakayetaka. Kama unakumbuka Yesu aliwaambia wanafunzi wake kuwa mtafanya mambo niliofanya na hata zaidi ya hayo mtafanya. Hii kauli inatuonyesha hakuna aliombwa kufanya manyonge kila mtu kwa jinsi yake aliumbawa afanye makubwa.
Jambo la muhimu jivike vazi la unyenyekevu ili upate kibali cha kufanya mambo makubwa na ya juu.
Na Henry Nicholaus
Barikiwa Sana


EVERY OPPORTUNITY THAT COMES IN YOUR LIFE  IS THERE FOR PURPOSE

Neno 'Purpose' ni neno la Kiingereza lenye maana ya KUSUDI au MPANGO.

Esta alikuwa ni mwana wa Abihaili Mbenjmini aliyekuwa akilelewa na Modekai baada ya wazazi wake kufa. Akiwa anaishi uhamishoni yeye na wayahudi wenzake. Siku moja Mfalme Ahusuero alimtaka Malkia Vashti acheze mbele yake lakini Malkia huyo alikataa. Hivyo ikamfanya Mfalme agadhibike mno hata akaona awaite wenye hekima ili wamshauri la kufanya Est 1:13-21. Nao walimshauri achague Malkia mwingine. Ndipo jambo hili likawa jema machoni pa Mfalme hata ikatolewa mbiu katika mikoa yote wanawake wapite mbele za mfalme Est 2:1-15

Hivyo basi Esta alichaguliwa kuwa rasmi kuwa Malkia katika uchaguzi wa Mfalme. Jambo hili halikueleweka vizuri kwa Esta kwa maana alidhani ni jambo la kawaida kwa Mfalme kuchagua yule anayemtaka asijue iko sababu maalum inayompeleka huko kwa Mfalme. Lakini ulipotimu wakati wa kusudi la Bwana basi Mungu alimfunulua ni sababu ya yeye kuchaguliwa kuwa Malkia kwa njia ya Modekai mjomba wake Est 4:12-14.

Hivyo watu wengi wanapopata nafasi mahali popote wanashindwa kujiuliza kwa nini wako hapo. Matokeo yake wanajikuta wakivuna hasara na uharibifu katika eneo waliopo hususani kwa vijana ambao hutoka vyuoni na kuingia kazini kwa sababu ya  kutokutambua kwao basi wanajikuta hata ajira yao ikiingia dosari.

Kila kitu duniani kinaendeshwa na Mpango wa Mungu hilo jambo watakiwa ulijue. Ukifahamu hili jambo utakuwa umeshinda maisha yako kwa zaidi ya asilimia 70 hivyo ni muhimu kujiuliza kwanza kwa nini niko mahali fulani na sio kwingineko. Hilo litakuwa la muhimu maana litakupa dira kuwa katika unachokifanya basi ukifanye kwa weledi mkubwa.

Hakuna mtu ambaye yuko duniani kwa hasara. Na hakuna linalotokea kinyume na Mpango wa Mungu labda mtu alivuruge mwenyewe maana Mungu alitupa nafasi ya kuamua. Tunatakiwa kuwa makini tukiwa mashuleni, makazini, vyuoni au kwengineko tujifunze kujiuliza kuhusiana na kusudi la Mungu katika yote yaliopo ndani yetu.

Na Henry Nicholaus
Barikiwa Sana


MBINU ZA KUKUSAIDIA KUOMBA VIZURI KWA MUDA MREFU

1. CHAGUA MAHALI PAZURI PA UTULIVU. *Mk 1:35
ili uweze kuomba kwa utulivu na kwa umakini, chagua au tafuta mahali pazuri
patakapokupa utulivu katika kuomba (concentration in prayer). Ndio maana Mungu
alipenda kuongea na Musa juu ya mlima. (Kut 24:12-18). Hata Yesu alizoea kwenda
kuombea mlimani, mahali palipo mbali na vurugu za watu, alipenda kwenda mlimani.
(Math 14:22-23). Tafuta mahali patulivu; chumbani, kanisani, mlimani (Math 6:5-6)

2. CHAGUA MUDA MZURI. *Mhu 3:1,7
Ili uweze kuomba kwa umakini mzuri, chagua muda mzuri ambao akili yako ma mwili
wako viko fresh. Usilazimishe kuomba hata kama akili yako au mwili wako umechoka sana. Kila jambo lina wakati wake. Kama umechoka sana, huo si muda wa kuomba, bali wa kupumzika. Usilazimishe ratiba. ni bora upumzike ili baadaye uweze kuomba vizuri baadaye. Usije ukajikuta unamkemea Yesu badala shetani. Penda kuomba wakati una nguvu ya akili na mwili, ili uwe makini kuongea na Mungu kwa akili timamu. Ndio maana Yesu alipenda kuamka alfajiri sana kwenda kuomba mlimani. (Mk 1:35, Luka 4:42)

3. OMBA KATIKA ROHO (NENA KWA LUGHA). *Efe 6:18, Rum 8:26-27
Mbinu nyingine nzuri ya kuomba kwa muda mrefu na kwa ufanisi, ni kuomba kwa Roho; yaani kuomba kwa kunena kwa lugha. Tunapoomba kwa akili za kibinadamu, Mungu anasikia pia, lakini maombi yako yanakuwa na mipaka / limited kwasababu akili ya mtu haijui kila kitu. Bali Roho wa Mungu anajua kila kitu. Naye hutupa kipawa cha kuomba kwa lugha ya mbinguni iliyo bora zaidi.(Yuda 1:20, Mk 16:17, 1Kor 14:1-4, 15-16,7)

4. OMBA KWA KUFUNGA WAKATI MWINGINE. *Math 6:16-18
Kufunga kula kunasaidia kudhoofisha mwili, ili roho iwe makini zaidi kuongea na Mungu kwa kina zaidi. Mwili huu siku zote haupendi kufanya mambo ya Mungu. Na mwili ukiwa umeshiba, unakuwa na uchovu na uzito wa kufanya mambo ya kiroho. Mbinu mojawapo ya kuudhibiti, ni kuunyima/kuupunguzia posho yake ya chakula. Mwili ukidhoofika kiasi, roho yako inapata nguvu na upenyo mzuri zaidi (Zab 35:13). Mashujaa wote wa imani walifunga na kuomba. Ndio maana Yesu anasema ‘mfungapo’ akimaanisha ratiba ya kufunga, ipo. Inasaidia.

5. OMBA NA RAFIKI (PRAYER PARTNER). *Mhu 4:9-10
Neno la Mungu linasema, ni heri wawili kuliko mmoja. Kuna faida ya kuomba pamoja na rafiki yako. Kwanza, mnapokuwa wawili au watatu, inaleta hamasa na ari ya kuomba zaidi. Si rahisi kujisikia mvivu unapokuwa na waombaji wenzako. Pili; nguvu ya kiroho inaongezeka. Neno linasema, mwombaji mmoja anafukuza adui elfu moja, bali wakiwa wawili, wanafukuza (sio elfu mbili) bali elfu kumi! Shangaa! (Kumb 32:20) Hiyo ni kanuni ya mbinguni/kanuni ya Ki-Mungu. Kadri mnavyoongezeka, nguvu ya Mungu huongezeka.

Kwahiyo, wakati mwingine, omba na rafiki yako, unayemwamini, unayeweza kumshirikisha mambo yako ya binafsi. Mashujaa wengi wa imani, walikuwa na marafiki wa kiroho. (Prayer Partners). Kwa Mfano:- Math 17:1-9

Musa - alikuwa na Joshua, Haruni na Huri
Eliya - alikuwa na Elisha
Daniel - alikuwa na Shadrack, Meshack na Abednego.
Yesu - alikuwa na Petro, Yakobo na Yohana.
Paul - alikuwa na Barnaba, Timotheo na Tito.
Wewe Je? Uko na nani katika urafiki wa kiroho?
Kama huna rafiki wa karibu wa kuomba naye, usikurupuke kujichaglia. Tulia umwombe Mungu akupe mtu atakayekuwa wa msaada kwako. Mtu mtakayefungamanishwa naye katika roho, hata kama mmetengana kijiografia, lakini katika roho, mko na umoja mzuri wa imani. (Math 18:18-19)

6. OMBA KATIKA MKAO UNAOKUPA UHURU NA NGUVU ZAIDI.
Katika kuomba kwa muda mrefu, mkao uliouzoea utakusaidia kwenda mwendo mrefu. Yakupasa kujua nguvu yako na udhaifu wako (strong point and weak point). Wakati wa kuomba, epuka mikao inayokuchosha haraka na tumia mikao inayokua nguvu zaidi. Kwa Mfano:- Ukiwa umechoka, usipende kuomba kwa kupiga magoti au kwa kuegemea kitandani. Ni bora uombe ukiwa umesimama au unatembea tembea, ili kuepuka usingizi na uchovu. Waombaji hodari wanaujua mikao inayowasaidia kuomba maombi marefu. Wengine hawana mikao maalum, bali wakiwa katika maombi, huwa wanabadilisha-badilisha mikao ili wasichoke. Hiyo ni mbinu nzuri pia.

Mifano ya Mashujaa wa Imani;
Ibrahim – aliomba kwa kusimama (Mwa 18:22)
Daniel - aliomba kwa kupiga magoti (Dan 6:10)
Paul - aliomba kwa kupiga magoti (Efe 3:14)
Yesu - aliomba kwa kulala chini (Math 26:38-39)
Eliya - aliomba kwa kukaa chini na
kuweka kichwa kati ya miguu (1Fal 18:42)
Mimi - huwa napenda kuomba kwa kutembea tembea
Naweza kumaliza kilomita nyingi chumbani kwangu
Nikitembea huku nikiomba.

Wewe Je? Unaujua mkao wa nguvu? Kama hujui, Tafuta kujua.

7.OMBA NA MUZIKI LAINI KWA KUMWABUDU MUNGU.
Muziki wa kiroho, na wataratibu, unaweza kukutengenezea mazingira mazuri sana ya kuomba kwa muda mrefu. Muziki wa kuabudu, unavuta uwepo wa Mungu kwa namna ya pekee. Neno linasema, waimbaji na wanamuziki walipoimba na muziki ukapigwa, nao wakawa kama mtu mmoja, utukufu wa Mungu ukashuka na kulijaza lile hekalu hata makuhani hawakuweza tena kuhudumu (2Nyak 5:12-14). Kule mbinguni, kila malaika wa sifa, ana kinubi (zeze/gitaa). Elisha hakutoa unabii, mpaka mpiga kinubi alipopiga kwa ustadi, ndipo mkono wa Bwana (Roho wa Mungu) alipokija juu yake, naye akatabiri.

Najaribu kukuonyesha, kuna connection kati ya muziki wa kiroho na utukufu wa Mungu. Kwahiyo, ukiweza kuomba huku umeweka kanda au CD ya nyimbo za kiroho za taratibu, utapata (experience) hamasa ya kiroho (motivation) na utasikia una nguvu ya kuomba kwa muda mrefu. Kama unaweza, tengeneza kanda au CD maalum yenye nyimbo nzuri unazozipenda wewe, ili uwe unaipiga wakati wa maombi. Utajikuta unaweza kuomba kwa muda mrefu na kwa bubujiko zuri Zaidi

Barikiwa sana


NAFASI YA MWANAMKE KIBIBLIA.

Friday, December 26, 2014

7:37 PM

Mwanzo 1:27 ‘Mungu akaumba mtu kwa mfano wake,kwa mfano wa Mungu alimwumba,mwanaume na mwanamke aliwaumba. Sikiliza mahali popote pale mwanamke ni mtu mwenye nguvu na ushawishi mkubwa katika kufanya mambo kuliko hata mwanaume.Ikiwa ushawishi huu utatumiwa katika mpango wa Mungu basi kusudi la Mungu litatekelezwa
Mungu hakumwumba mwanamke kwa bahati mbaya au makosa,kila ambacho Mungu alikifanya ,alikifanya kwa kusudi kwa lugha nyingine kila ambacho Mungu alikifanya maana yake moja kina nafasi mbele zake na mbili kuna wajibu ambao Mungu aliweka ili utekelezwe na hicho kitu.

Lengo la ujumbe huu ni kukueleza nafasi ambayo Mungu amempa mwanamke katika kanisa,jamii,nchi,ndoa na nk na wajibu wa yeye kutekeleza katika nafasi hiyo:-

1.Mungu anamtazama mwanamke kama msaidizi wa mumewe . Mwanzo 2:18 “Bwana Mungu akasema si vyema huyo mtu awe peke yake,nitamfanyia msaidizi wa kufanana naye”. Tangu kuumbwa kwa Adam,mpaka Mungu kumletea Eva inasemekana miaka mingi ilipita hapa katikati.Sasa tunajua katika ile sura ya kwanza na ya pili ya kitabu cha mwanzo,Mungu alikuwa amempa Adam wajibu wa kutekeleza.
Ikafika wakati Mungu akaona ule wajibu ni mkubwa sana kwa Adam kuutekelekeza ndipo akampa Eva.Kitu Mungu anataka tujue hapa ni hiki,wajibu aliopewa Adam peke yake asingeweza kuutekeleza bila Eva,maana yake nafasi ya Eva kwa Adam ilikuwa ni ya muhimu zaidi.Pasipo Eva,Adam angeshindwa kutekeleza wajibu
Sasa hata leo katika ndoa,kanisa Mungu ameweka wanawake ili wawe wasaidizi katika majukumu ambayo Mungu amewapa na waume zao au wachungaji wao makanisani.

2. Mwanamke kama mlinzi wa agano na kusudi la Mungu. Mithali 14:1 “ Kila mwanamke aliye na hekima hujenga nyumba yake ; bali aliye mpumbavu huibomoa kwa mikono yake mwenyewe” , Mwanzo 3;13 “ Bwana Mungu akamwambia mwanamke ,nini hili ulilolifanya ? Mwanamke akasema nyoka alinidanganya ,nikala”..

Ndoa ni agano la Mungu kwa wanadamu. Mlinzi wa agano kimsingi ni mwanamke. Mara nyingi shetani akitaka kuvuruga ndoa atatafuta mpenyo au nafasi hiyo kwa mwanamke ili asambaratishe ndoa hiyo.Sasa mwanamke yupo ili kulinda kusudi hilo.Asipokaa kwenye nafasi yake ya ulinzi basi ajue kwamba kusudi la Mungu la kuwaunganisha halitatimia.

Nisikilize ndoa yoyote inapovuruguka ujue mwanamke hakusimama vema kwenye nafasi yake ya ulinzi. Ngoja nikuonyeshe kitu hiki. Adam na Eva walipokula tunda ambalo Mungu aliwaambia wasile , kila mmoja wao aliulizwa swali lake. Adamu aliulizwa uko wapi? Mwanzo 3:9, na Eva alimwambia Mwanamke ni nini hili ulilolifanya , Mwanzo 3:13.Ipo tofauti kubwa sana katika haya maswali mawili.Swali la Adam lilimaanisha kwa nini haupo kwenye nafasi yako? Na swali la Eva lilivuka hapo na kumaanisha kwa nini hujafanya ulilotakiwa kufanya yaani kulinda agano.Mahali popote mwanamke ulipo ikiwa ni katika ndoa ,kanisa ,jamii,nchi, jifunze kulinda kusudi la Mungu ambalo unajua Mungu amekuagiza . jifunze kupitia mama yake Musa , yeye alilinda agano la wana wa wa Israeli kwa kumficha Musa na kuhakikisha hafi maana alijua Musa hakuzaliwa kwa bahati mbaya. Kutoka 2:1-10.

3.mwanamke kama muombolezaji.
Luka 23;27-28 “Mkutano mkubwa wa watu wakamfuata na wanawake waliokuwa wakijipiga vifiua na kumuombolezea , Yesu akawageukia akasema ,Enyi binti za Yerusalemu ,msinillie mimi bali jililieni nafsi zenu na watoto wenu”.Sikliliza , Mungu amweapa kinamama uwezo mkubwa wa kuomboleza kwa ajili ya mahitaji mbalimbali ndani ya jamii ,ndoa, kanisa, nchi nk. Hivyo Mungu anamuhesabu mwanamke kama muombolezaji.

Hii ina maana kama kuna vitu havijakaa sawasawa kwenye ndoa,kanisa,nchi nk, Mungu anajua mwanamke atasimama kwenye nafasi yake na kuomba ili Mungu apate kuliponya taifa kupitia maombi .Ukiona maasi mengi yamezidi katika taifa mfano, vijana wa kike kutoa mimba, uasherati,uchafu na uzinzi basi ujue kina mama katika mji au taifa hawajasimama vizuri kwenye nafasi zao. Si kana kwamba nawalaaumu mama zangu na dada zangu kwa kusema hivyo,bali ninachotaka niwaonyeshe ni kwamba usalama na maendeleo mazuri ya vijana wa kike na kiume katika familia,kanisa na taifa kwa ujumla upo katika mikono yenu na ndio maana Yesu aliwaambia mjililie ninyi na hao vijana wenu.

Nikuulize swali , jiulize una watoto wangapi? Tabia na mwenendo wao ukoje? Je ni mzuri? Unambariki Mungu? sivyo jiulize chanzo cha tabia hizo kwa mwananao ni nini au ni nani aliyehusika na tabia hiyo? Najua unaweza kwa haraka kusema ni shetani au kumtupia lawama mmeo. Sikiliza Shatani huwa hafanyi chochote isipokuwa pale anapokuwa  amepewa nafasi na mtu au watu fulani , kwa kifupi mtu anaposhindwa kusimama kwenye nafasi yake. Sasa ukisoma vizuri Biblia utagundua nafasi ambayo Mungu amempa  mwanamke kwa habari ya watoto wake, ndoa yake, kanisa lake kwa ujumla.Jifunze kusimama kwenye nafasi yako, funga na kuomba kwa ajili ya taifa hili ili Bwana Mungu apate kuliponya . maombi yako yatasababisha kutengenezwa kwa mahali palipobomoka na krejeshwa kwa njia za kukalia. 

4.Mwanamke kama mlinzi wa nafsi ya mtoto wake wa kiume .
Katika hii sura ya 31 ya kitabu cha Mithali tunaona habari za mama mmoja ambaye alikuwa na mtoto wa kiume na huyu mtoto alikuwa ni mfalme. Ule mstari wa pili unasema “ Ni nini mwanangu ?, tena ,nini mwana wa tumbo langu? Tena nini mwana wa nadhiri zangu ? Usiwape wanawake nguvu zako; wala moyo wako usiwape wale waharibuo wafalme”. kinamama wakijua namna ya kuzikamata nafsi za watoto wao wa kiume ,nakuambia kuna uwezekano mkubwa kabisa hawa watoto wasifanye tendo la ndoa mpaka watakapo kuja kuoa.Hili litawezekana pale tu kinamama watapofanikiwa kuzikamata na kukaa kwenye nafsi za watoto wao wa kiume.Huyu mama alimuuliza maswali mengi mwanawe kwa sababu aliona nafasi yake mama kwenye nafsi ya mwanawe inanyang’anywa na wanawake wengine.Naamini waraka huu mfupi na wa kwanza utafanyika kuwa msaada kwa wamama wengi mahala popote pale.

Neema ya Bwana wetu Yesu Kristo na iwe pamoja nanyi.

Na; Patrick samson Sanga.


MUNGU HUJIBU MAOMBI YETU SAWASAWA NA TUMJUAVYO

Isa 59:1 inatueleza kuwa Mungu husikia maombi yetu yote tuyaombayo kwake. Tena hana humsikiliza kila mtu kwa kadiri ya mahitaji yake. Tumefundishwa Tuombe pasipo kukata tamaa   Lk 18:1 inatuambiwa kuwa imetupasa kumwomba Mungu pasipo kukata tamaa hii ina maana kuwa kuna uwezekano wa kuomba na kutopokea majibu.

Kwa nini tunaweza tukaomba na tusipokee majibu au yakaja ya design tofauti na yale tuliyo yaomba. Hii ni kwa sababu yeye Mungu humjibu mtu sawasawa na jinsi mtu amjuavyo Mungu. Efe 3:20 inasema kuwa "Basi atukuzwe yeye awezaye kufanya mambo ya ajabu mno kuliko yoe tuyaombayo au tuyawazayo, kwa kadiri ya nguvu itendayo kazi ndani yetu."

Kwa hiyo siku zote Mungu hujibu maombi yetu tatizo ni kiwango cha sisi kuweza kupokea majibu hayo kama NGUVU ITENDAYO KAZI ndani yetu ni ndogo basi hata kupokea kwetu majibu kutakuwa kwa kiwango cha udogo. Ili sasa tuweze kujiweka katika eneo au 'position' nzuri ya kupokea kile tukiombacho lazima tumekeze katika kumjua Mungu Yn 17:3 Uzima wa milele uko katika kumjua Mungu na hii ndio nguvu itendayo kazi. Huwezi kumtumikia Bwana usiye mjua. Watu wengi hawamfahamu Mungu kwa sababu wao ni watu wa Jumapili.

Pasipo kutoa nafasi moyo wako umjue Mungu hasara itaendelea kubaki kwako. Maana sio Mungu mwenye shida hivyo unapozidi kumjua Mungu ndivyo unavyozidi kupokea majibu katika maombi yako.

Henry Nicholaus
Barikiwa sana


JE UMEWAHI KUJIULIZA KUWA SIKUKUU YA KRISMASI INA MAANA GANI KWAKO.
Watu wengi wamekuwa wakiisherekea sikukuu ya Krismasi kwa mazoea kwani wengi huhakikisha wanakwenda kanisani hata kama si mazoea yake ukimuuliza atakuambia kuwa Yesu amezaliwa. Kwa hiyo utaona kuwa ni mazoea ndio yanayomsukuma kufanya hivyo kama ana watoto pia inawezekana akawa hata mkali kwao kama hawatakwenda siku hiyo. Utaona jambo hili limetoka kwa wazazi ambao wamerithisha jambo hili. Sio mbaya ni vizuri lakini jambo la muhimu si tu mtu aende kanisani bali afahamu kwa nini anakwenda.Wengine huuandaa hata vitu vizuri kama vyakula vya kutamanika. Lakini ukifahamu maana yake unakuwa zaidi mno na mnufaikaji mkubwa wa sikukuu hii.
Yn 1: 1-12 anaeleza jambo hili kwa mapana mno. Yesu alizaliwa la kwanza ambalo watakiwa kulijua kuwa Mungu anakupenda kuliko hata unavyodhani. Upendo wa Mungu katika maisha yetu ni mkubwa. Fikiri licha ya dhambi tulizofanya bado Mungu hajatuacha. Haya yanadhihirishwa mno na Yn 3:16 Mungu aliupenda ulimwengu hata akamtoa mwanawe wa pekee ili kila amwaminie asipotee bali awe na uzima wa milele. Mpango wa Mungu uwe na uzima ndani yako ndio maana ameamua kumwachilia Yesu aje ili sisi tupokee uzima. Huu ni upendo wa ajabu maana anatupenda bila sababu. Maana huwezi kumfanyia mtu mabaya halafu bado akaendelea kukupenda.
Lakini jambo la pili ni habari za kizazi kipya. Kuzaliwa kwa Bwana wetu Yesu kunatuambia na kutukumbusha kuwa kuna kizazi kipya ambacho Kristo kwa kuzaliwa kwake kiliundwa na Yohana amelieleza hili lakini si wengi ambao wamemwelewa.Unaposoma biblia yako hebu angalia Yn 1:11-13. Katika kifungu hiki kinaonyesha kuwa kuna watu ambao wameonyesha kumpokea alipozaliwa naye aliamua kuwapa kibali cha kuwa wana wa Mungu. Mstari wa 13 unaeleza kuwa mwana wa Mungu kuna maana gani? Anaeleza waliozaliwa si kwa damu wala kwa mapenzi ya mwili. Kama tulianza kuzaliwa kwa mwili na Yesu akaamua kutupeleka katika ngazi nyingine uwe na uhakika kuna kuzaliwa kwa mara ya pili ambako ndiko kunatufanya sisi tuwe na kizazi tofauti na cha ulimwengu.
Tofauti ya kizazi hiki na kile cha ulimwengu ni kwamba kizazi hiki hakitegemei dunia kuendesha maisha yao. Na huku ndiko nilipopata somo la uchumi wa mbinguni. Na nikafahamu kuwa kama vile kuna uchumi wa mbinguni basi kuna fursa ambazo ni za waaminio na sio kila mtu.
Mpendwa nichukue fursa hii nikujulishe kuwa inapofika siku ya Krismas unatakiwa kuiangalia kwenye mtazamo huu na ndipo utakapositawi sana maana utakuwa unaelewa mpango wa Mungu juu ya maisha yako Yer 29:11
Na Henry Nicholaus
Barikiwa Sana


KWA NINI TUAMINI

Imani ni kuwa na hakika ya mambo ya tarajiwayo ni bayana ya mambo yasiyoonekana Ebr 11:1. Wakati Mungu anaumba dunia alitumia imani kufanya vitu ambavyo leo sisi tunavitumia. Hivyo basi kila kitu tunacholiona ni matokeo ya imani. Kwa maana hiyo basi imani huwezi kuitenganisha imani na uumbaji wa Mungu.

Unaposoma biblia yako kuanzia Mw 1:1-25 utaona Mungu anatumia neno la imani kufanya vinavyoonekana. Roho Mtakatifu alitulia juu ya vilindi vya uso wa maji ili aatamie kile alichokuwa na anahitaji kufanya Mungu. Ndipo tunaona Mungu anasema na iwe nuru, na kwengineko anaendelea kusema vivyo hivyo.

Mungu aliumba vitu tunavyoviona kutoka katika  ukiwa, tena utupu na giza Mw 1:2. Hivyo basi sisi kama wakristo wa leo ni muhimu tukaamini maana tusipoamini hatutaweza kuendana na maisha humu duniani kwani tutaona ni mahali pa gumu mno kwa mtu kuweza kuishi na sio kweli kwamba ni mahali pagumu ili kinachohitajika ni kufuata utaratibu tu. Kama vinavyokuzunguka ni zao la imani basi anayevitumia hawezi kukwepa kwenda kinyume na imani.

Hii ndio sababu kubwa ambayo ilimfanya Mungu atembee na Ibrahimu kwa imani. Fikiri Mungu anamwambia Ibrahimu aende katika nchi aliomwamuru na Ibrahimu hakuwa akiijua lakini Ibrahimu alifuata maelekezo yote Mungu aliokuwa akimpa Mw 12:1 ni jambo gumu kufanya maelekezo ya mambo usiyoyajua lakini Ibrahimu alijua kuwa anaishi kwenye dunia iliyoumbwa kwa imani hivyo imani haikwepeki.

Angalia watu wengi wamejikuta katika eneo gumu mno katika maisha hii ni kwa sababu ya hawana imani. Ndugu mpendwa katika maisha tulionayo sasa jifunze kukaa katika imani ili mambo yasikusumbue wala usipate shida yeyote.Tunashindwa hata kupokea uponyaji hali tu wagonjwa kwa sababu hatuna imani. Tunashindwa kuvuta ahadi alizotupa Mungu kwa sababu hatuna imani. Hivyo utaona akosaye imani hujiweka katika nafasi mbaya ya kukosa mengi katika dunia ya leo.

Na Henry Nicholaus
Barikiwa Sana 


MUNGU AMEKUPA NAFASI YA UAMUZI JUU YA YALE ALIYOWEKA WAZI MBELE ZAKO.

Katika kichwa cha habari kuna mambo mawili makubwa nayo ni 'uamuzi' na 'wazi'.Uamuzi ni ile hali ya kufikia hitimisho ya jambo fulani. Inawezekana iwe ni mtu mmoja au wengi. Na kwa nini hii ni kwa sababu hatuwezi kushughulika na mambo ambayo hatuyajui. Mambo yaliyo wazi ni yetu sisi Kumb 29:29

2Fal 20:1-6 Hezekia alikuwa mgonjwa lakini alipooambiwa na Isaya nabii kuwa atakufa kama asipotengeneza mambo yake. Basi alimkumkumbusha Mungu namna yeye alivyokwenda katika kweli naye Mungu alimpa jibu kwa njia ya Isaya na kumwambia kuwa atampa miaka mingine na kumponya ugonjwa na pia atauweka ufalme wake imara. Hezekia alihojiana na Mungu. Alitumia nafasi aliopata kuamua mustakabali wake wa baadae.

Watu wengi huishia katika malalamiko badala ya kufanya maamuzi katika nafasi ambayo Mungu amewapa. Na matokeo yake kutafunywa na matatizo kila wakati. Mungu hafanyi kitu duniani bila kumshirikisha mtu. Si kwa sababu hana nguvu la hasha Yeye ni mwenye nguvu mno bali Yeye ni mnyenyekevu na hufuata utaratibu hata kama vyote ni vyake Zab 24:1. Japokuwa ametupa tuwe mawakili hivyo hutumii nafasi yake kufanya mambo bali amejiwekea utaratibu Ufu 3:20.

Hakuna kitu duniani kitatokea mtu asijue, sema tatizo ni kwamba wale wanaoambiwa wanashindwa kuelewa maana yake maana huweza kuja kwa mafumbo au wanashindwa kujua kama yaliosema yametoka kwenye kinywa cha Mungu au 'illusion' Amo 3:7. Mfano mtu mmoja alifahamishwa kuwa kuna mtu anakufa lakini yule wa kwanza akashindwa kumsaidia yule mlengwa hata kwa maombi. Mungu akambebesha mwingine naye akafanya vilevile ikawa imesalia wiki moja akamweleza jirani yake. Yule jirani akawa anasikia msukumo wa kumwambia lakini hakumweleza kitu hata yule mtu akafa pasipo msaada kwa maana waliopewa taarifa hawakuwajibika.

Huwezi kwenda mahakamani ukaambiwa jitetee ukasema mimi sijatoa rushwa. Sawa yamkini hujatoa rushwa lakini lete hoja ili tuamini kuwa hujatoa rushwa. Ukikaa kimya utahesabika kuwa na hatia kisha hatua zitachukuliwa. Hata kwa Mungu zinahitajika hoja na sio simulizi Isa 43:26. Leteni hoja zenye nguvu asema Bwana. Mshawishi Mungu kwa yale unayoyataka kupitia hoja. Na sio uishie kulalamika kuwa Mungu hakuoni kumbe wewe hujitendei haki.

Angalia mifano ya mahojiano yaliofanyika huko nyuma kati ya watu na Mungu
Suleimani na Mungu   2Nya 1:7-12
Gideoni na Malaika     Amu 6:11-18
Musa na Mungu          Hes 14:11-20

Chukua uamuzi wa kufanya maamuzi na sio kulalamika. Usichukue muda wa maombi kama mda wa kawaida. Bali ni mda wa thamani wenye nguvu kubwa ya kuamua mustakabali wako.

Na Henry Nicholaus
Barikiwa Sana.


UMUHIMU WA KUMPOKEA ROHO MTAKATIFU

Matendo ya Mitume 1:8 Lakini mtapokea nguvu, akiisha kuwajilia juu yenu Roho Mtakatifu; nanyi mtakuwa mashahidi wangu katika Yerusalemu, na katika Uyahudi wote, na Samaria, na hata mwisho wa nchi.

Ukiwa na Roho Mtakatifu unapokea uweza tofauti na ule wa mtu wa kawaida. Ndio maana neno la Mungu linasema "Lakini mtapokea nguvu" kama Yesu alisha tuokoa kwa nini tena tupate nguvu kwa maana wokovu wake unatosha? Hii kwa sababu ili tupate kukamilishwa tunakamilika kwa njia ya Roho Mtakatifu. Kumbuka pale Mwanzo 1:26 maandiko yanasema "Mungu akasema, Na tumfanye mtu kwa mfano wetu, kwa sura yetu… " Hivyo kuna uwingi ulio katika umoja aliouzungumzia Mungu. Sasa basi tunakamilika kama nafsi zote za Mungu zitakuwa ndani yetu.

Jambo la pili unaposoma neno hili kutoka Mdo 1:8 linasema "…nanyi mtakuwa mashihidi wangu katika Yerusalemu, na katika uyahudi na Samaria, na hata mwisho wa nchi." Hii ina maana kuwa licha ya wanafunzi wa Yesu kutembea naye na kumjua lakini wao bado hawakuwa mashahidi maana hawakukamilisha na Mungu. Hivyo pale tunapopokea nguvu za Roho Mtakatifu ndipo tunapokuwa wakristo.

Watu wengi wanaenda kanisani na kuitana wakristo lakini wasipate kujua kuwa wao si wakristo. Maana wakristo wana Roho wa kweli. Kwa sababu si watu wote wapendao kuwa na nguvu za Roho Mtakatifu bali wengine huona sawa tu bora kanisani anafika basi hufikiri kuwa yeye ni mkristo kwa sababu pia alibatizwa. Tujiulize kwa nini Yesu alisema wako ambao atawakana siku ile na kutowajua. Hii ina maana kuwa wako watu wanakwenda kanisani au kutumika kanisani pasipo kukamilishwa na hiki ndicho kigezo ambacho kinawafanya wakae mbali na Mungu Rum 8:9b.

Roho Mtakatifu ana faida nyingi ndio maana Yesu alimleta kwetu.Zifuatazo ni faida za kuwa na Roho Mtakatifu.

  1. Roho Mtakatifu hutuombea Rum 8:26b
  2. Roho Mtakatifu hutueleza habari za mambo yajayo Yn 16:13
  3. Roho Mtakatifu hutusaidia kuomba ipasavyo Rum 8:26
  4. Roho Mtakatifu hutushuhudia sisi ni wana wa Mungu Rum 8:14
  5. Roho Mtakatifu hutusaidia kutembea katika njia iliyo sawasawa Rum 8:9
  6. Roho Mtakatifu ni Mwalimu Mwema 1Kor 2:12-13

Na Roho Mtakatifu hawezi kutenganishwa na Mungu maana ni nafsi ya Mungu au Yesu 1Kor 12:b. Ni muhimu ndugu mpendwa kama hujampokea Roho Mtakatifu ufanye sasa. Ziko faida nyingi lakini kwa sehemu nimeainisha hizo.

Na Henry Nicholaus
Barikiwa Sana


HAKUNA UKRISTO BILA NGUVU YA MUNGU



Hauwezi Kumtenganisha Mkristo Na Nguvu Ya Mungu, Ni Sawa Na Samaki Na Maji, Sawa Na Mizizi Na Ardhi, Ama Pumzi Na Mtu!“Bali Wote Waliompokea Aliwapa Uwezo [Nguvu] Ya Kufanyika Wana Wa Mungu, Ndio Wale Waliaminio Jina Lake” (Yohana 1:12)

Hauwezi Kuwa Mkristo na Kuishi Maisha Ya Ushindi Dhidi Ya Shetani, Dhambi Na Changamoto Kama Hauna Nguvu Ya Mungu!Hatuokoki Kwa Kusema Tu Maneno Midomoni BILA NGUVU YA KUTUFANYA WANA WA MUNGU, Katu na Abadani! Kama Huna Nguvu Ya Mungu, Wokovu Hauwezekani… Kuishinda Dunia na Tamaa Zake Kwako huo Utakuwa Ni Msamiati Mgumu!Ndio Maana Mtu Wa DINI (Mshika Dini, Mapokeo Na Taratibu za Wanadamu) Hawezi Kuamini Kwamba Mtu Anaweza Kuokoka Akiwa Duniani, Hii Ni Kwa Sababu Mtu Wa Dini Hajakutana Na NGUVU YA MUNGU Inayotufanya Sisi WALIOOKOKA Kuwa INVISIBLE… Anadhani Kwa sababu Yeye ameshindwa Kumshinda Shetani Na Dhambi na tamaa za Dunia Hii, Na Wengine wote tumeshindwa!
Asikudanganye Mtu, Nguvu Ya Mungu Inapatikana Bure Kwa Mungu Mwenyewe… Mwenye Kiu aje Anywe Bure, Aje Anunue Divai (Roho Mtakatifu) na Maziwa (Neno) (Isaya 55:1-2, Yohana 7:37-39)!

Nguvu Ya Mungu tunaipata wapi?
  1. Kwenye Neno Lake          Waebrania 4:12 “Kwa Maana Neno La Mungu LI HAI, TENA LINA NGUVU…” Yohana 1:3 “Vitu Vyote Vilifanyika Kwa NENO LA MUNGU. Pasipo NENO HAKUNA CHOCHOTE KILICHOFANYIKA” Yeremia 23:29 “NENO LA MUNGU NI KAMA MOTO, NI KAMA NYUNDO IPONDAYO MIAMBA KUIFANYA VIPANDE VIPANDE” Kama Ukiamua Kutumia MUDA WAKO, NGUVU YAKO, GHARAMA YAKO YA KIFEDHA nk Kutafuta NENO LA MUNGU Utakutana Na Nguvu Ya Mungu Ya Kubadili Maisha Yako! Tumia Muda wako: Kujisomea Mwenyewe NENO LA MUNGU Kwenye Biblia Yako. Pia Kama Kuna SEMINA Za Neno la Mungu Na Mafundisho Usikose… Wekeza Muda Wako katika Neno Utakutana Na Nguvu ya Kuyabadili Maisha Yako! Tumia PESA YAKO Kununua VITABU VYA WATUMISHI WA MUNGU VYA MAFUNDISHO Mbalimbali Ya Neno La Mungu… Nunua CD, DVD Za Mafundisho Ya Neno La Mungu Kwa Kadri Mungu atakavyo kuwezesha… Nakuhakikishia Ukiweka Pesa Yako Katika Neno lililo Kwenye Vitabu Na CD, DVD Za Watumishi Wa Mungu WALIOITWA NA WALIOTUMWA NA MUNGU, Maisha Yako Hayatabaki vile yalivyokuwa!.

  1. Maombi         Wekeza Muda Wako Kwenye Maombi. Zama tulizomo Hizi Ni za Hatari sana. Shetani yuko Kazini Kuliko Wakati Mwingine Wowote. Tuko Katika Nyakati za Mwisho. Ni nyakati ambazo wale walio MAKINI KWENYE MAOMBI Na Kumsikiliza Mungu WATASALIMIKA. Hakikisha Unakuwa na Muda Wa Kutosha Kwenye Maombi. Usisingizie kwamba Uko Busy au Muda haupo. Huu ni UONGO WA IBILISI. KUNA MAMBO MENGI UNAFANYA YASIYO NA TIJA Ambayo kama UKIYAACHA au KUPUNGUZA MUDA WAKE, Utapata muda wa kutosha wa KUOMBA. Kuna Wakristo Wengi kuomba Hata NUSU saa tu kwao ni kazi sana. Ni sawa na ADHABU. Lakini kwa kweli ni mbinu ya SHETANI TU hii. MAMBO YA KUOMBEA NI MENGI SANA; Familia yako (ndoa; mme/mkeo, watoto), dada na kaka zako, ndugu wengine ulionao, Kanisa lako, Watu waokoke, Yesu apate heshima yake, miujiza, ishara na maajabu viwepo kwenye Ibada zenu, Maisha yako pia yanategemea sana maombi yako kwenda kule ambako Mungu anatamani yaende. Kama Hauombei Maisha yako, Unamruhusu Shetani aingilie na kupitisha AGENDA zake za UHARIBIFU, KUIBA NA KUCHINJA (Yohana 10:10), Unapoyaombea Maisha yako UNAJIWEKEA ULINZI (Zaburi 32:6, Mathayo 26:41-44), Ombea TAIFA LAKO; Mambo yote mabaya au mazuri ndani ya taifa lako ni matokeo ya ULIMWENGU WA ROHO; UKIOMBA UTABADILI NCHI YAKO, UTALIPONYA TAIFA LAKO (2 Nyakati 7:14)

  1. Kufunga              Jitahidi Uanze Kujizoeza MAOMBI YA KUFUNGA pia; anza kwa kufunga maombi ya saa 12 (asubuhi hadi jioni)… walau hata mara 2 au 3 kwa wiki. Halafu baada ya hapo Mungu atakusaidia kuweza Kufunga maombi ya Siku nzima (masaa 24), baadaye utakavyozidi kukomaa utaweza kufunga siku 3, 7 nk kutegemea maendeleo yako katika SHULE YA MAOMBI NA KUFUNGA. KUFUNGA NA KUOMBA HUACHILIA NGUVU NA UPAKO WA KUVUNJA Vifungo vya Kiroho kama LAANA, DHAMBI, KUTOFANIKIWA nk (Isaya 58:5-9)

  1. Ushirika Wako Na Roho Mtakatifu        “Neema Ya Bwana Wetu Yesu Kristo, Na Upendo Wa Mungu Baba, NA USHIRIKA WA ROHO MTAKATIFU, Ukae pamoja nasi, sasa na hata milele, amen” (2Wakorintho 13:14) Roho Mtakatifu Ni: Mwalimu: Anatufundisha mambo yote ( Yohana 14:26, 1Yohana 2:27) Kiongozi: Anatuongoza Na Kututia katika Kweli Yote (Yohana 16:13-15, Warumi 8:9-16) Shahidi: Anatushuhudia juu ya dhambi tukikosea au kutenda dhambi na kutukumbusha kutubu LAKINI Pia Anatushuhudia mioyoni mwetu kuwa sisi ni WANA WA MUNGU (Yohana 16:7-8, Warumi 8:16) Msaidizi: Roho Mtakatifu Ni Msaidizi wetu, anatusaidia kuyaendesha maisha ya Imani kwa uhakika na ushindi (Yohana 14:16) Roho Mtakatifu ni Roho Wa NGUVU, UWEZA, SHAURI, HEKIMA, UFAHAMU, UCHAJI MUNGU, UPENDO, KIASI ( Isaya 11:1-2, 2Timotheo 1:7) Tangu Siku ya Pentekoste, ROHO MTAKATIFU yuko Hapa Duniani, Anakaa na WAAMINI, ANAKAA NDANI YAO( Yohana 14:17)

Utakavyozidi KUMPA NAFASI, KUMPENDA, KUMTHAMINI na KUWA NA USHIRIKA NAYE, Utafurahia NGUVU YA MUNGU muda wote! (TAFADHALI CHUKUA BIBLIA YAKO NA USOME MISTARI YOTE NILIYOANDIKA KATIKA STATUS HII) Ubarikiwe!

 
HATA KAMA MAZINGIRA HAYAONYESHI KUFANIKIWA KWA KILE AKUAMBIACHO BWANA USIOGOPE AU USIONE HOFU KUKITEKELEZA
Katika maisha tulionayo tumekuwa tukizoea kuomba katika nyakati tofauti za maisha ili kuhakikisha tunapata mahitaji yetu. Mara nyingi ahadi au majibu ya Mungu huwa hayafanani na mazingira yanamzunguka yule anayeipoke au wao wanaozipokea. Na huu ni utaratibu ambao Mungu amejiwekea yeye mwenyewe kwenye ulimwengu wa roho kama ulivyo ule utaratibu wa mzaliwa wa kwanza ili atukuzwe na kuinuliwa kwa kila kitakacho tendeka ili hata wale wasiomwamini wafahamu kuwa iko nguvu isiyo ya kawaida iliosababisha.
Mfano Ibrahimu alipokuwa akitaka kujua kutoka kwa Mungu kuwa ni nani atakayemrithi kwa kuwa yeye ni mzee tena hana mtoto. Mungu akamweleza kuwa atakayemrithi atatoka katika kiiuno chake na jambo la ajabu akamweleza kuwa uzao wake utakuwa kama nyota za mbinguni Mw 15:2-7. Ni majibu ya Mungu ambayo kwa hali ya kimwili unaweza kuona kuwa hayawezekani. Na jambo hili yamkini lilimpa shaka Ibrahim hata kuzaa na mjakazi wake maana aliposhauriwa na mkewe amwingilie mjakazi wake hakuona shida kuliko Mungu alichomsemezesha Mw 16:1-4.
Lakini licha ya majibu ya Mungu kwa Ibrahimu kuonekana kama ya mzaha katika Mw 18:9-14 tunaona ujumbe wa malaika wanampa Ibrahimu habari njema juu ya yeye kupata mtoto siku kama waliomtembelea mwakani. Haya ni majibu ya kushangaza na ndicho kilimfanya Sara acheke. Maana aliona kwa desturi ya wanawake mda wake wa kuzaa ulikuwa umekoma. Lakini kwa kuwa hakuna kinachoshindikana kwa Bwana mambo haya yalitukia.
Biblia pia inatueleza habari ya kuzaliwa kwa Yesu haikuwa tofauti na staili ya Mungu kuwajibu watu kile kitakachotokea baadae katika maisha yao. Marium anatokewa na Malaika anaelezwa kuwa atapata mimba kwa uweza wa Roho Mtakatifu ikumbukwe ijapokuwa Roho Mtakatifu alikuwa akifanya kazi lakini hakuwa amefunuliwa. Hivyo yalikuwa maelezo tata sana kwa Marium kuzaa pasipo kumjua mume.
Hata wewe leo yamkini Mungu amekusemezesha kupitia ndoto au maono. Na unaona kuwa alichokueleza hakiwezekani hebu badili fikra zako. Isa 55:8-9 inatueleza mawazo ya Mungu yako juu kuliko yale ya mwanadamu. Pale tunapokoma kufikiri ndipo Mungu anapoanzia. Hivyo majibu ya Mungu ni muhimu tukayatafakari katika staili ya imani na hii ndio itatuwezesha kumwelewa. Habakuki alipokuwa akimwomba Mungu kwa manuny'uniko kwa nini matajiri wananyanyasa watu wake. Mungu akamwambia Habakuki kuwa "Mwenye haki ataishi kwa imani".
Hivyo ni muhimu kutembea katika imani iliuelewe njia za Mungu. Maana kwa kufanya hivyo utakuwa ukitembea na kuishi kwa staili ya maisha ya ulimwengu wa roho.
Na Henry Nicholaus
Barikiwa Sana


ILI UWEZE KUFANIKIWA LAZIMA UKAE CHINI YA UONGOZI

Ili uweze kuwa mtu fulani baadae unahitaji kukaa chini ya mtu fulani mwenye haiba hiyo ambayo una maono nayo hapo baadae ili aweze kukufundisha kukaa katika dizaini ya maono ulionayo. Unataka kuwa mhandisi kaa chini ya mwandisi, unataka kuwa mfanyabiashara kaa chini ya mfanyabiashara, unataka kuwa mwalimu kaa chini ya mwalimu.

Yos 1:1-2 anampa jukumu Yoshua kama mtumishi wa Musa. Tunapojiuliza kwa nini Mungu aliamua kumtazama Yoshua kama mtumishi wa Musa wakati alipokuwa akimbebesha kusudi lake. Tunapata na majibu na kuelewa kuwa Mungu alitaka sisi tujue kuwa hakuna namna twaweza kuwa vile twataka kuwa kama hatuta kaa chini ya uongozi wa watu wa haiba ya maono yetu. Tazama Yoshua anafanyika kuwa nabii sababu tu alikuwa akikaa chini ya Musa na kwa jinsi hii inawezekana kabisa alijifunza namna ya kutembea na kuishi kama nabii. Unajua ukiwa profesa huwezi kutembea kama mtu wa kawaida kuna aina ya dizaini ya kuishi kiprofesa.

Jambo hili tunaliona pia kwa Elisha unabii wake ulikuja kwa kuwa alikaa chini ya Eliya 2Fal 2:2-6, 11-15. Usione shida kukaa chini ya watu. Usipende kujiona wewe ni mjuzi wa mambo mengi kaa kwanza ufundishwe ili upate kuongezeka hata katika kile unachokifahamu. Elisha hakuacha kumfuata Eliya katika kifungu cha maneno nilichokuandikia utaona kila wakati Eliya alipokuwa akimwambia Elisha kuwa Mungu amemwambia aende mahali fulani utaona Elisha hakukubali kumwacha Eliya hii ni sababu kuwa alitaka unabii. Naye alifahamu moyoni mwake kuwa akitaka kuwa nabii lazima akae chini ya nabii.

Vile vile tunaona Paulo naye wakati Yesu amemkomboa katika giza na kumketisha katika ufalme wa pendo lake. Akahitaji watu waweze kumfundisha Paulo namna ya kuweza kutembea katika utume. Na ndipo tunaona Mungu anamtuma Anania aende akamwekee mikono Paulo Mdo 9:17-18. Baada ya hapo Paulo anawekwa chini ya uongozi wa Barnaba ambaye ndiye alimtambulisha kwa mitume Mdo 9:27.

Mpendwa ni fursa kubwa mno kukaa chini ya uongozi wa watu. Maana hata Yesu alipokuja alihitaji kukaa chini ya uongozi ya watu fulani ili apate kutimiza lile ambalo Mungu amelikusudia kwa wanadamu nalo ndilo Agano Jipya ambalo tunaishi ndani ya hilo.

Na Henry Nicholaus
Barikiwa Sana



KWA NINI WATU WENGI HAWANA MSUKUMO WA MUNGU NDANI YAO

Ukiangalia watu wengi katika dunia ya leo hususani vijana hawana msukumo wa Mungu ndani yao. Utagundua kuwa mara nyingi wao huona kila kitu kuwa ni sawa. Semina za neno la Mungu zinaandaliwa kila kona lakini huwezi kuwakuta. Vitu vingi vizuri vinaandaliwa kwa gharama lakini hawahudhurii. Utakuta wanashabikia mambo ambayo ni kweli si yenye kumwinua Mungu mfano mabishano ya siasa, mabishano ya mpira, kuongelea,kusikiliza ama kucheza miziki ya kidunia, kuzungumzia wanawake kama ni wanaume au kuzungumzia wanaume kama ni wanawake.

Sasa leo tutaona sababu kwa nini watu wamekuwa wakiishi maisha ya dizaini hii
Watu wengi wanaishi kwenye mazingira ambayo hayawezi kumruhusu Mungu aingilie maisha yao. Tukisoma 2Tim 3:1-5 tunaona jinsi kizazi cha leo kinavyoishi. Paulo amefafanua vizuri juu ya maisha yaliopo katika kizazi cha leo kwa jinsi ile huwezi kuona mtu akipata msukumo wa Mungu ndani yake. Badala yake atakuwa na msukumo wa vile vitu ambavyo anaviishia ndio maana unaweza kukutana na mtu akakuambia anasikia hamu ya kunywa pombe au kuvuta sigara. Hii ni kwa sababu amezoea kuishi kwenye mazingira hayo tena ndio yanayompa msukumo.Hadi kijana anafikiri aende akaibe uwe na uhakika kuwa maisha anayoishi ndiyo yamemshurutisha kuwa wa namna ile.

Watu wengi hawana hazina ya kutosha ya Neno la Mungu. Huwezi kuishi maisha ya Mungu kama humjui Mungu. Utaweza kuisha pale utakapokuwa ukiweza kumfahamu Mungu. Kol 3:16 anatueleza kuwa Neno la Mungu nalikae kwa wingi mioyoni mwetu. Ukikosa Neno la Mungu huwezi kuwa na msukumo wa Mungu kwa kuwa huna kinachoweza kukuongoza katika njia ya Mungu. Msingi wa msukumo wa Mungu uko kwenye Neno lake. Ndio maana Daudi anasema kuwa Neno la Bwana ni taa na mwanga wa njia zake Zab 119:105. Kwa hiyo ukiwa na Neno lake unajua wapi kwa kupita na kwa jinsi hiyo Mungu atakuwa upande wako.

Ili sasa uweze kuwa na msukumo wa Mungu ndani ya maisha yako kila siku na kila wakati wekeza vya kutosha kwenye neno la Mungu na kisha kwepa kuwepo au kukaa kwenye mazingira ambayo yanaweza kukupa shida au kukwamisha mahusiano yako na Bwana Isa 57:2 maovu yetu yametufarakanisha sisi na Mungu hata tusiuone uso wake.  Ni wazi kama tukikaa katika Bwana ni lazima tutakuwa na msukumo wa kuhudhuria semina au hata kuomba. Maana inawezekana siku yako inapita lakini huombi.

Unaweza kupitia mistari hii pia ikakuwezesha kuona kwa mapana kile kilichokuwa ninakizungumza 1Tim 4:1, Yos 1:8, Zab 119:9-11

Na Henry Nicholaus
Barikiwa Sana

 
YESU ANATAZAMIA UFANIKIWE MAANA AMEKWISHA KUBARIKI
Watu wengi twaweza kufikiri kuwa kutofanikiwa kwetu ni mpango wa Mungu katika maisha yetu. Unajua sisi ni mabalozi wa Bwana. Na kwa kuwa hakuna balozi anayeweza kwenda ugenini kwa pesa au gharama zake mwenyewe kuhudumia taifa lake mahali pa ugeni hivyo basi hata sisi tulio wageni katika dunia hii inatupasa kutambua kuwa kama hatutaishi kutokana na gharama za Mungu hatutaweza kuishi.
Unaposoma Mw 9:1 tunaona mara baada ya Nuhu kutoka katika tufani ya gharika Mungu alimwambia yeye na wanawe wazae waongezeke. Mstari huu unaweza ukauangalia kibinadamu ukasema kuwa Mungu amesema wazaane sawa inaweza ikawa hivyo kwa namna moja ama nyingine lakini kusudi la Mungu ni sisi tufanikiwe katika roho zetu. Kwa maana nyingine maisha yetu yalete matunda sahihi sawasawa na kusudi la Mungu tuliobebeshwa.
Kwa hiyo tuache malalamiko kusema sio mpango wa Mungu. Tusipende kumsingizia Mungu mambo ambayo hakustahili kunyooshewa vidole tena yatupasa hata kumwomba toba kwa habari ya jambo tu kama hilo. Yer 29:11 inatueleza wazi nini nia ya Mungu juu ya maisha yetu akieleza kuwa anatuwazia mawaazo yalio mema ili katika siku za maisha yetu tuwe na tumaini siku zote.
3Yoh 1:2 unasema,"Mpenzi naomba ufanikiwe katika mambo yako yote na kuwa na afya yako kama vile roho yako ifanikiwavyo." Angali kwenye mstari huu Mungu ametumia neno 'yote' hii inaonyesha kuwa mpango wa Mungu wa kufanikiwa kwako haujafungwa katika mambo fulani ya maisha yako na mengine akayaacha hii inamaanisha kuwa mpango wa Mungu si baguzi katika maisha ya mtu bali mtu ndiye anayeamua ni maisha gani tena yenye kiwango gani ayaishi.
Kinachomfanya Mungu kutazamia kuona ukifanikiwa ni kwa sababu alipokuwa akiumba dunia aliumba na kuiweka katika nyakati na majira hivyo basi kwa maana hivyo anategemea baada ya muda fulani katika maisha basi maisha yako nayo yanatakiwa kufikia katika viwango fulani kutokana na muda alio uweka. 
Ndugu mpendwa baada ya kutumia muda kukuonyesha kuwa sio mpango wa Mungu wewe uwe fukara. Ndio maana Yesu anategemea akuone wewe ukifanikiwa katika mambo yako sasa ni muhimu ukawekeza maombi yako ili usamehema kama ndio ilikuwa mtazamo wako wa awali kuwa ni mpango wa Mungu uwe jinsi ulivyo pia uombe macho ya rohoni uone fursa ili upate kuongezeka.
Na Henry Nicholaus
Barikiwa Sana  

UMUHIMU WA NENO LA MUNGU

Bwana Yesu asifiwe mpendwa kila unapopita mahali pengi unasikia Neno la Mungu linahubiriwa inawezekana ni kwa njia ya redio, runinga au hata mtandao. Pengine pia ni mikutano ya hadhara, semina au makongamano. Je umewahi kujiuliza labda ni kwa nini neno la Mungu lihubiriwe kwa mapana hivyo katika siku za usoni.

Jambo la kwanza: Neno la Mungu latupa haki ya kuishi Mt 4:4. Biblia inasema kuwa hatutaishi kwa mkate bali kwa kila Neno litokalo kwenye kinywa cha Mungu. Hii inatueleza kuwa sio chakula ambacho wengi twaamini tukila tunapata nguvu bali ni Neno la Mungu linalotupa haki ya kuishi. Kwa maneno mengine ni kwamba Neno la Mungu ndio lenye mustakabali wa mwisho wa kuishi kwetu.

Jambo la pili: Neno la Mungu latupa imani Rum 10:31. Imani ni kuwa na hakika ya mambo yatarajiwayo ni bayana ya mambo yasioonekana Ebr 11:1. Bila kuwa na uhakika wa mambo yatajiwayo mtu hawezi kuishi maana dunia iliundwa kwa imani. Ndio maana Biblia inasema mwenye haki wangu ataishi kwa imani. Imani inatokana na kusikia kwako Neno la Mungu usiposikia huwezi kuwa nayo.

Jambo la tatu: Neno la Mungu latutakasa Yn 17:17.Biblia inaposema habari za Neno la Mungu kuwa makini ukiangalia ni lipi ambalo linaonyeshwa kwako. Kwa maana hata Neno la Mungu ni Yesu mwenyewe hivyo angali kwa makini ni msukumo upi Mungu anaachilia kupitia achakokueleza. Hivyo kupitia Neno la Mungu tunasafishika.

Jambo la nne: Neno la Mungu latupa uzima Yn 17:3. Uzima wa milele uko katika katika Neno la Mungu Biblia inafafanua kuwa uzima wa milele ndio huu wakujue wewe ni Mungu wa kweli na Yesu Kristo mwanawe ulie mtuma. Kwa hiyo uzima wa milele hauko mbinguni ila katika watu. Hutegemeana na kiwango au kipimo cha kumjua yeye.

Jambo la tano: Neno la Mungu latupa uhuru. Uhuru ni ile hali ya mtu kuwa na maamuzi ya mwisho juu ya mambo yake binafsi.Kuna aina tatu za uhuru nazo ni uhuru, uhuru kweli na uhuru kweli kweli. Kipimo chetu cha kumfahamu Mungu ni kipimo cha uhuru wetu. Hivyo uhuru wa mtu umefungwa katika mapana ya mtu kumjua Mungu.

Hivyo ndugu mpendwa kwa muda mchache ambao tumepata kwa pamoja ni matumaini yangu kuwa utawekeza vya kutosha juu ya Neno la Mungu. Maana sasa umetambua nini umuhimu wa Neno la Mungu linalohubiriwa kila mahali.

Henry Nicholaus
Barikiwa Sana.

 
KUNA VITU VINGI AMBAVYO YESU ANAPENDA KUKUSEMEZESHA. JE UMEWEKEZA KWA KIASI GANI KUHAKIKISHA UNAMSIKIA VYAKUTOSHA?
Je wajua Mungu anayoshauku kubwa ya kukuambia vitu vingi lakini mkao uliokuwa nao unamkwaza hata yeye kushindwa kuachilia kile alichonacho kwa ajili yako.
Yn 16:12-13 unasema "Ninayo mambo mengi yakuwaambia lakini hamwezi kustahimili hivi sasa. Lakini yeye atakapokuja, huyo Roho wa kweli, atawaongoza awatie kwenye kweli yote; kwa maana hatanena kwa shauri lake mwenyewe, lakini yote atakayoyasikia atayanena, na mambo yajayo atawapasha habari zake."
Hivyo nia ya Mungu ni sisi tumfahamu yeye kwa mapana makubwa ndio maana anavitu vya kutushirikisha au kutueleza. Swali letu kutoka kwenye kichwa cha somo linasema "Je umewekeza kwa kiasi gani kuhakikisha unamsikia vyakutosha?
Kumjua Mungu ni uzima wa milele hivyo usipokuwa na utaratibu wa kujitengea Muda kwa ajili ya kumsikia Mungu hatuwezi kuwa na uzima ndani yetu. Uzima hukaa ndani ya mtu kama akimjua Mungu na kumjua Mungu huja kwa kumsikia yeye. Inawezekana kupitia semina, mafundisho kanisani au hata mahubiri katika mikutano ya hadhara.
Ni muhimu kuhakikisha unakaa katika eneo zuri ambalo litamshawishi Mungu kuachilia kile kilichopo ndani yake. Mfano kukaa mbali na dhambi biblia inasema kupitia Isa 59:2 Lakini maovu yetu ndio yametufarakanisha sisi na Mungu hata tushindwe kuuona uso wake. Hivyo kama tutashindwa kuona uso wake si jambo lakuwezekana yeye kukusemezesha maana utakuwa umekaa mahali ambapo ni tofauti na pale alipo.
Maisha ya toba ni muhimu kwa maana pasipo toba hatuwezi kuwa safi Mungu alimwambia Musa avue kiatu chake maana mahali alipo ni patakatifu hii ina maana kama tunataka kukutana na Mungu kwa njia yeyeote ile basi kusafisha ni jambo la Muhimu lizingatiwe.
Jifunze kusoma neno la Mungu ili upate kukaa karibu na Mungu. Kwa maana kwa kuisikia sauti ya Mungu basi tunapata kumjua yeye siku hata siku. Muda wa kuwekeza ni sasa na sio baadae chukua hatua leo ili upate kuwa salama.
Na Henry Nicholaus
Barikiwa Sana

 MUNGU ANATAKA USHIRIKA NA WEWE NA SIO UMWONE KAMA MUNGU WA MSAADA

"Unaposoma Yn 3:16 inasema "kwa maana jinsi hii Mungu aliupenda ulimwengu hata akamtoa mwanawe pekee, ili kila amwaminiye asipotee, bali awe na uzima wa milele."

Mungu anataka uwe na ushirika na yeye. Watu wengi wanataka Mungu awe msaada wao tu. Unakuta mtu kwa sababu ya shida anaamua kumtafuta Mungu kwa bidii yamkini anasumbuliwa na magonjwa au matatizo mbalimbali.

Lakini pale anapokuwa amepokea uponyaji basi anaachana na Mungu na kuendelea na njia zake kana kwamba ayafanyayo haya mwisho. Yuko kijana mmoja kanisani kwetu alikuwa hana ajira akawa akihudhuria kanisa kweli lakini mara baada ya kupata ajira akaachana na kanisa. Siku mmoja tulimwomba mkewe tufanye ibada kwake alituambia yeye ataondoka huo wakati ikiwa ni sababu ya kutuepuka tu.

Hivyo watu wengi wana desturi ya kumfanya Mungu kama Baba wa msaada ambavyo yeye hatamani tumtazame kwa mtazamo huo.Mungu anahitaji ushirika na wewe kwa kiingereza 'FELLOWSHIP' na sio umwone kama sehemu ya msaada.

Fellowship au ushirika maana yake ni mahusiano mapana kati yako na Bwana hii ina maana kutii mapenzi yake kwa kulitii neno pamoja na kushukuru. Fellowship pia ni zaidi ya mahusiano maana Mungu mwenyewe hufanya makazi ndani ya mtu na kuketi naye pamoja.

Hivyo kwa ufafanuzi huo mfupi kuhusu fellowship sasa utaweza kuelewa kwa nini fellowship na sio vinginevyo ndio maana hata Christina Shusho aliimba kuwa 'anataka ushirika na Roho' Hata hivyo utaona ni msukumo gani mkubwa uliokuwepo katika kutafuta fellowship na Mungu.

Ndugu mpendwa kama ndio mazoea uliokuwa nayo acha maana athari yake ni kubwa. Naomba nikuulize swali uliwahi kuona watu wanakwenda kwenye semina mtumishi habadiliki lakini yeye hapokei uponyaji anakuja mtu siku ya kumalizika semina na anapokea uponyaji. Sababu kubwa ni hii. Geuza mtazamo wako juu ya Mungu anza upya maana humkubali yeye anyenyekeaye.

Na Henry Nicholaus
Barikiwa Sana              

 
JIFUNZE KUSOMA VITABU VYA ELIMU YA MUNGU ILI UPATE KUJUA MAMBO YALIOFICHIKA
Hatuwezi jua mengi kama sio wasomaji wazuri wa vitabu. Siri ya kuwa na ufahamu mwingi ni kujua mengi. Dan 9:1-2 Danieli agundua mda wana wa Israeli kukaa uhamishoni ulikuwa umekwisha kwa sababu ya kusoma vitabu.
Kama unapenda maarifa ni muhimu ukajijengea mazoea ya kuanza kusoma vitabu vingi. Ndio maana mwanafunzi hushauriwa kusoma vitabu vingi ili awe katika nafasi nzuri si tu ya kujibu mtihani bali hata ya kuufaulu mtihani huo.
Watu wengi wameweka uvivu wakingoja wasikie na hiki ndio kinachoendelea mno duniani, mtu hawezi kusoma biblia mpaka angoje Jumapili ifike asomewe kanisani au asikie mahubiri. Hii ndio inayowapa nguvu hususani manabii wa uongo maana wamejua kuwa watu wapendi kusoma biblia hivyo wavisemavyo huwaaminisha watu hata wakadhani kuwa ni kweli Mungu alisema na wengi husema "IMEANDIKWA' lakini hataji mstari siasa gani hizi ndani ya kanisa.
Njia pekee ya kuondokana na ujinga ni usomaji wa neno la Mungu na vitabu mbalimbali waandikavyo watumishi kupitia biblia hivyo ni vyema ukawekeza muda wako huko maana huo muda hautakuwa wa hasara hata kidogo.
Tuondoe uvivu ili tuweze kujua na kufahamu mambo mengi ambayo hatuyajui. Unajua hata watu hawaoni nyakati za mwisho kwa sababu vitabu kama biblia sio sehemu yao bali wao na maisha tu. Danieli kwa kujua kuwa muda wa kukaa utumwani ulikuwa miaka sabini tena umekwisha alianza kuchukua hatua. Huwezi kuchukua hatua yeyote kama hujui chochote.
Ili ubadili maisha yako anza kujenga nidhamu ya kusoma vitabu nawe utashangaa maisha yako yakipata maendeleo kwa njia ya mabadiliko. Chukua hatua……………………………………………….!
Na Henry Nicholaus
Barikiwa Sana

 
ULICHONACHO NI CHA THAMANI KULIKO UNGEWEZA KUFIKIRI
Watu wengi huwa hujiona maskini kwa sababu hawana fedha. Siku zote ukiujadili umaskini kwa viwango vya fedha utakutesa. Mimi yaweza kusema umaskini ni ile hali ya ukosefu wa maarifa, uwezo au ufahamu juu ya mambo au kitu. Na kwa sababu ya mitazamo yao ya umaskini kama ukosefu wa fedha imewagharimu mno pasipo wa kujua kwa muda sasa.
Kut 4:1-4 Mungu alimwambia Musa nini ulichanacho mkononi? Hii ina maana una kitu ambacho ni cha thamani lakini bado hujakitambua. Musa alipoambiwa aitupe ile fimbo chini iwe nyoka ndipo akajua kuwa alikuwa na uwezo mkubwa licha ya yeye kuona kama hataweza kwenda kwa Farao.
Usipojua una nini ni ngumu kuweza kunasuka kutoka katika wimbi la umaskini hivyo basi kujitambua kuna nafasi kubwa ya kuweza kukufanya ufanikiwe ama usifanikiwe. Usipojitambua hutakuwa mgeni wa mtu. Jambo hili ni tatizo kwa wanafunzi wa vyuo vikuu wakidhani kuwa serikali ndio itakayo wapa kazi. Hali imetokana na wengi kushindwa kujitambua. Soma hata historia serikali nyingi duniani haziko kwa ajili ya watu bali kwa ajili ya maslahi fulani.
Hebu tazama serikali ya Marekani inavyotumia fedha nyingi kwenye jeshi lakini kwa nini serikali yao imeshindwa kuwapatia wamerikani wote bima ya afya. Wamarekani walio matajiri ndio wawezao kumudu gharama za afya bali wale maskini hawawezi. Mpaka hapa utaona nini lengo la serikali nyingi duniani.
Ondokana na tabia ya malalamiko juu ya serikali angalia una nini kisha kitumie kile ulichonacho natamani ujue kuwa Mungu hakukuleta duniani kama pipa lisilo nakitu bali aliweka hazina ndani yako. Kuwa na muda peke yako kuweza kujitathimini vya kutosha ili uweze kujua ni wapi uweze kusimama.
Mfano mimi na wenzangu watatu tuliweza kutengeneza gazeti la shule. Jambo hili lilishindikana kwa muda mrefu pale shuleni. Lakini sisi tulichukua 'RISK' hivyo tukaweza kutengeneza gazeti kwa mara ya kwanza. Hivyo nikutoe hofu wewe mwenye mawazo ya kitu hebu yathibitishe kwenye uhalisia.
Na Henry Nicholaus
Barikiwa Sana
NI KWA NINI WAKRISTO WANAE MUNGU ALIYE HAI LAKINI WANAISHI MAISHA YA SHIDA

Imekuwa ni jambo la kawaida sasa kuona walokole wakiishi maisha ya hali ya chini hali wanamtumikia Mungu kwa bidii. Jambo hili tunapata ufafanuzi kutoka Mw 3:8-9 inasema "Kisha wakasikia sauti ya Bwana Mungu, akitembea bustanini wakati wa jua kupunga Adamu na mkewe wakajificha kati ya miti ya bustani, Bwana Mungu asiwaone.Bwana Mungu akamwita, Adamu uko wapi?"

Adamu na mkewe waliposikia sauti ya Mungu walijificha hii inaonyesha kuwa dhambi huzaa uoga. Hivyo wakristo wengi kwa sababu ya kuishi maisha ya dhambi wamejikuta wakijenga uoga juu ya mambo mbalimbali. Kama woga wa kujaribu. Wengi wanashindwa kusubutu kwenye maisha yao jambo ambalo ni tatizo kubwa. Na woga ndio kikwazo kikubwa cha maendeleo.

Mara baada ya Adamu kujificha yeye na mkewe Mungu hakuwaona tena. Sikiliza huleta giza kila wakati. Hivyo unapokuwa ndani yake basi wakaa gizani na hii ndio sababu Mungu hakuwaona sio kwamba kimwili hajui walipo bali kiroho walihama kutoka kwenye nuru mpaka kwenye giza ambako huko ilikuwa ngumu yeye kuonekana tena.

Na ndio sababu Mungu alimwita Adamu uko wapi. Hii ilikuwa na maana kuwa mahali ambapo alizoea kumwona Adamu hamwoni tena. Hivyo tatizo letu wakristo ni kwamba mahali tulipo ndio kikwazo na mahali hapo pamesababishwa na dhambi maana Isa 59:2 inasema lakini maovu yenu yamewafarakanisha nyinyi na Mungu hata msiweze kuuona uso wake.

Ndugu mpendwa kama unapenda kufanikiwa penda kuishi maisha yasiyo laumika. Maisha yasiyo laumika haya ni maisha ndani ya Yesu Kristo. Hapo ndipo utakuwa umekaa mahali sahihi kukutana na Mungu au kuzungumza nae.

Na Henry Nicholaus
Barikiwa sana

USIPOCHUKUA HATUA ZA KUMWOMBEA EVA WAKO SHETANI ATABADILISHA MPANGO WA MUNGU JUU YA MAISHA YAKO

Watu wengi wanafahamu kuwa jukumu la kuoa au kuolewa huanzia pale wakati wa 'courtship' unapofika. Hili ndio kosa ambalo wanafanya na ndio maana ndoa nyingi zinafungwa na watu ambao sio sahihi kwa mtazamo kuwa wana pesa. Ikiwa sio 'creteria' sahihi ya uchaguzi ya wapendanao. Pia kusita tumeona ndoa zikivunjika kama pipi siku za karibuni huku harusi zao zikiwa zimegharimu pesa nyingi.

Tukitazama mazungumzo ya Ibrahimu na Sara Mw 16:1-4 utaona Sara anamshauri mumewe amwingile Hajiri mjakazi wao ili wajipatie mwana. Ikuumbukwe kuwa wakati huo Mungu alishamwahidi Ibrahimu kuwa atampa mtoto Mw 15:3-7. Lakini kwa sababu Ibrahimu aliambiwa yeye na biblia haituambii kama alichoambiwa na Mungu alimshirikisha mkewe au hata alichukua muda kumwomba Mungu ili alichoambiwa mkewe hata pasipo kusikiwa aridhie.

Hivyo ilisababisha mwanya ambao shetani alitumia kwa njia ya Sara ambapo alitumia njia ya ushawishi alionao Sara kwa mumewe kufanya jambo ambalo yeye Mungu halikumpendeza. Hivyo kwa Ibrahimu kumwingia Hajiri kulisababisha kuingiliwa kwa mpango wa Mungu kuinua kizazi kitakatifu kupitia uzao wake.

Jambo hili hili liliendelea kwa Yakobo ambapo yale yaliofanywa na bibie ndio yalioendelea kwake mkewe Rahaeli alimshawishi amwingilie Bilha mjakazi wake ili ajipatie mtoto kwa yeye. Hivyo utaona kilele kinaendelea kwa Yakobo jambo hili liliharibu mpango wa Mungu wa kujiinulia kizazi kitakatifu kwa Yakobo Mw 30:1-5.

Samsoni naye aliingia kwenye kosa hili pia biblia haijatuambia kama alikuwa na muda wa kumwombea Delila wake hii ilimfanya shetani apate nguvu kwa njia ya wafilisti ili wamwangushe Samsoni na alifanikiwa kumshawishi na kujua asili ya nguvu zake. Ambapo aliwaeleza wafilisti kisha wakamtoboa macho.Hivyo utaona Samsoni anagharimika na mpango wa Mungu unaharika tu kwa kushindwa kumwombea Delila wake hata akamsaliti Amu 16:1-22.

Usikimbilie kupenda tu hebu omba kwanza kwa ajili ya Eva wako ili uepukane na madhara yanayo epukika. Mke mwema hutoka kwa Bwana hivyo unapokaa magotini utapata mke sahihi ambaye ataweza kulea shauri la Bwana katika maisha yako pasipo usumbufu. Usifikiri ukimsikiliza Mungu utakosa wazuri, wazuri wapo usiwe na haraka nao we vumilia na tena watu wa Mungu ndio wenye wake wazuri.

Ndugu mpendwa we anza leo kuomba kwa ajili ya Eva wako usiangalie una muda mrefu kiasi gani mbele yako kumbuka maombi huwekwa hazina hilo usisahau

Na Henry Nicholaus
Barikiwa Sana

 
KILA JAMBO/TUKIO LINALOTOKEA LIMEKUWA NA UJUMBE NYUMA YAKE
Kuzaliwa kwa Bwana Yesu ni moja ya jambo ama tukio ambalo lilitokea kipindi cha nyuma. Tunaona habari zake Luka 2:7.Lakini kama unafuatilia kwa karibu mno kuzaliwa kwa Yesu kulikuja kwa mpango kamili Lk 2:11 biblia inatueleza aliyezaliwa ni Mwokozi.Lakini licha ya kujua hiki bado twatakiwa kujua nini je nini sababu ya kuwepo huyo mwokozi? Hilo ni la muhimu mno.
Katika kuzaliwa kwa Yesu tunaona uanzishwaji wa kizazi kipya. Hapo awali tulikuwa katika kizazi cha Adamu lakini baada ya Adamu kutenda kosa.Yesu akaja kututenganisha na hiyo asili ili tusitende dhambi na ndipo kizazi kipya kinapotokea 1Petro 2:9 inasema Bali nyinyi ni mzao mteule….. Hivyo unagundua kuwa kuzaliwa kwa Yesu kuliaachilia kitu nyuma yake hakukutokea kwa namna ya kawaida bali kulitokea kwa mapenzi ya Mungu yaliodhahiri ili mwanadamu apate wokovu
Kufa kwa Bwana Yesu pale msalabani ni pia moja ya tukio. Mara baada ya kufa Yesu pale msalabani kurasa moja ilifungwa na nyingine ikafunguliwa na si wengi wanao jua kuwa kuna kurasa ambayo ilifungwa na nyingine mpya kufunguliwa. Kudondoka kwa damu ya Yesu pale msalabani ilikuwa ni ishara kubwa ikimaanisha AGANO JIPYA. Watu wengi wanadhani agano jipya linaanzia wakati Yesu alipozaliwa sio kweli maana bado ile laana aliolaaniwa Adamu haikufutika.
Mw 3:17-19 utaona ile laana aliopewa Adamu lakini kuzaliwa kwa Yesu hakukusababisha ile laana ifutwe bali kufa kwake ambako damu yake ilitumika kama kafara ili wokovu upatikane ndio maana damu yake ili nyunyizika ardhini mahali ambapo laana iliwekwa.
Situ hilo unaposoma Lk 23:45 inasema jua limepungua nuru yake pazia la hekalu likapasuka. Hii ilikuwa inaashiria kuwa swala kuhubiri Injili sio tena la wale waliokwenye huduma tano za kanisa yaani manabii, mitume, wainjilisti, wachungaji na waalimu. Bali ya watu wote. Kwenda madhabahuni hataenda kuhani tu bali kila mtu.Maana zamani zile patakatifu patakatifu aliingia kuhani tu.
Hivyo basi yako mengi sana ambayo yamefichika katika kuzaliwa na kufa kwa Bwana wetu Yesu Kristo nami kwa neema ya Mungu nimejadili na wewe kwa sehemu tu ili uweze kuona kuwa uko umuhimu wa wewe kuhakikisha unajua ni mambo gani yamefichika katika matukio.
Iko misiba inatokea kwenye familia watu wanashindwa kujua ni mambo gani katika familia zao yamefungwa na yapi yamefunguliwa.Mfano Nyerere alipokufa ukurasa wa siasa za kijamaa ulifungwa na kuinua siasa za utandawazi. Nelson Mandela alipokufa maraisi wote duniani walikusanyika hii ni kuonyesha uko ukurasa duniani ulifungwa na uko ukurasa ulifunguliwa.
Yer 33:3 anasema umwite Bwana naye ataitika atakuonyesha mambo makubwa usiyo yajua hivyo muulize Mungu yanayotokea Tanzania, kwenye familia yako, au kazini ama shuleni yanaashiria nini?
Na Henry Nicholaus
Barikiwa Sana

WEKA BIDII KATIKA KUMTAFUTA BWANA

Unaposoma Luka 19:1-5 unakutana na habari ya mtu mmoja tajiri jina lake Zakayo. Huyu alikuwa na shauku ya kumwona Yesu. Lakini ikiwa ni tofauti sana kwa hali ya kawaida kwa sababu ya ufupi alionao aliamua kupanda juu ya mkuyu.

Tukiangalia sehemu hii ya maneno jambo la kwanza ambalo limeonekana ni 'SHAUKU' au kwa kiingereza 'DESIRE'.Zakayo alikuwa na shauku ndani ya moyo wake. Je wewe mpendwa unayesoma somo hili unayo shauku ya kukutana na Yesu? Kama ndio mbona unaangalia movies na miziki siku nzima bila hata kugusa biblia?

Kitakachokufanya umwone Yesu ni kiwango cha utayari ulichonacho juu yake. Maana Zakayo utayari wake ndio uliomfanya aweke utajiri pembeni na kuivaa aibu ila tu akutane na Yesu. Je wewe kaka wa leo ulie sharobaro utayaweza hebu chukua kwa mapana kitendo cha Zakayo licha ya heshima ya utajiri aliokuwa nao aliamua juu ya mkuyu hii ni aibu kwa hali ya kawaida lakini Zakayo hakuiangalia.

Fikiri tu hata ushuhuda kuutoa inakupa shida je waweza kufanya jambo lakijasiri kama hili. Yesu alisema mtu akitaka kunitumikia ajitwike msalaba wake amfuate. Hivyo kukutana na Yesu ni gharama maana kunahitaji uweke muda wa semina, self-bible reading na hata muda wa maombi.

Hivyo pasipo kuweka juhudi ni ngumu kuweza kukutana na Yesu maana ufalme wa mbinguni unatekwa na wenye nguvu. Hivyo ni vyema ukaanza na moyo wako kwanza maana kimtokacho mtu ni kile kiujazacho moyo wake.Maana Zakayo aliyafanya yale yaujazayo moyo wake ndio maana aliweka aibu pembeni.

Yesu alisema njia iendayo uzimani imesongwa songwa hivyo basi ni muhimu uhakikishe unaweka jitihada maana sio rahisi kuipita

Na Henry Nicholaus
Barikiwa Sana

 
IT IS NOT OVER YET
Ninashangazwa na baadhi ya wakristo namna wanavyo kubali kushindwa pale wanapokutana na changamoto katika maisha.Unachotakiwa kuelewa wewe kama mtoto wa Mungu wewe si mhanga wa matatizo na hili linaelezwa vizuri na Habakuki licha ya changamoto alizopata alichagua kufurahi "Walakini nitamfurahia Bwana nitamshangilia Mungu wa wokovu wangu Yehova aliye Bwana ni nguvu zangu, Yeye huifanya miguu yangu kuwa kama kulungu, Naye ataniendesha katika mahali pangu palipoinuka" Hab 3:18
Kwa maneno mengine licha ya matatizo lakini Habakuki hakuyumbishwa na alichokiona, kisikia au kuhisi. Huu unatakiwa uwe mtazamo wako mpendwa. Chochote hakiwezi kutimia mpaka ushinde. Mambo yanaweza yasiende vizuri au namna ulivyokusudia hilo lisikupe tabu unachotakiwa ni kumwamini Mungu na kumsifu kama Habakuki alivyofanya. Sema ndani ya roho yako kuwa hutashindwa na kisha umtukuze Bwana.
Kumbuka Paulo na Sila licha ya kufungwa minyororo na kuwekwa gerezani walimsifu Mungu. Na hii ni hatua walioichukua na sio kulia na kuogopa. Unapokumbana na matatizo sio mda wa kulia bali ni muda muafaka wa kumwangalia Mungu alipo na kumsifu tena kwa kumrudishia utukufu. Hii ni siri ambayo wengi hawaijui Mdo 16:23-36.
Huu ni wakati wa wewe kumsifu Bwana kuliko ulivyokuwa ukimsifu huko nyuma. Unaweza wakati mwingine usihisi hata kufanya hivyo maadamu neno la Mungu ndilo lisemalo basi inakupasa ufanye tu kwa sababu huku ndiko ushindi wako ulipo.
Weka imani yako kw Bwana, mwabudu katika roho na kweli na atapokea sifa zako kisha ataachilia nguvu zake ziweze kukusaidia katika matatizo yako.
Barikiwa sana
Na Henry Nicholaus



No comments:

Post a Comment