Bwana Yesu asifiwe, kuanzia tarehe 1/1/2017 tutakuwa tukihamia katika website yetu iitwayo www.egospeltz.org

SPECIAL


MAFANIKIO HAYAJI KWA KUOMBEWA ILA KWA MBINU
Watu wengi wamekuwa wakiona mafanikio kama ndoto kwao kwa kuwa wameshindwa kupata ufahamu sahihi juu ya maisha ya kufanikiwa. Ni kweli watu wengi wamewekeza jitihada na juhudi nyingi katika kutafuta mafanikio ikiwemo na kuombewa au kuomba juu ya mafanikio lakini hiyo si misingi wa mafanikio. Leo nataka ujue misingi ya mafanikio ni mbinu ndio maana shule zikawepo. Watu wanafikiri tu akiweka juhudi anafanikiwa. Hayo si ya kweli. Juhudi ni jambo moja linalohitaji mbinu ili izae matunda.
Kila kitu duniani asili yake ni ulimwengu wa roho kuanzia mtu mpaka vitu anavyotumia kwa kusema hayo kila kitu kina roho ndani yake. Hivyo basi vitu hivi unahitajika uwe na ufahamu navyo nawe utavitumia utakavyo. Kwa kuwa vyote asili yake ni rohoni Paulo anatuambia wazi juu ya habari hizi  "Vaeni silaha za Mungu mpate kupinga hila za Shetani. Kwa maana kushindana kwetu si juu ya damu na nyama; bali juu ya falme na mamlaka, juu ya wakuu wa giza hili, juu ya majeshi ya pepo wabaya katika ulimwengu wa roho" Efe 6:11-12. Hivyo basi kama tunataka kufanikiwa lazima tujifunze mbingu za kiroho za kuvitawala.
Fikiria unafanya biashara na watu wa dini tofauti una uhakika kiasi gani juu ya njia wanazotumia kufanya biashara? Ili kupata riziki? Kama unataka kunielewa vizuri nenda kwenye maeneo yenye mfululizo wa vibanda vya chipsi utagundua licha ya wao kukaa sehemu moja bado mwisho wa siku wanapata vipato tofauti tena vyenye utofauti mkubwa. Utagundua wazi kwamba hawa jamaa wanatofautiana mbinu ambazo za msingi ni za ulimwengu wa roho. Ukiwafuatilia kila kitu wamelingana lakini tofauti yao iko kwenye mbinu za kuvuta wateja katika ulimwengu wa roho. Kwa kuwa watu ni roho hivyo hutumia mbinu za ulimwengu wa roho kuwapata. Hujawahi ona mtu anatoa mwanae kafara ili apate pesa. Hii ni kwa sababu mtu ni roho na anauhusiano na vitu vingine ndio maana anaweza kutumika kama kivutio cha pesa. Sisemi ufanye hivyo maana hii ni mbinu ya ufamle wa giza ziko za nuruni na ndizo Bwana anapenda tujifunze leo.
Nataka kukuuliza kufanikiwa kwa nchi ya China kuliletwa na maombi au mbinu haijalishi ni za madhabahu gani. Tuache kudanganyana kama unapenda kufanikiwa tafuta namna ya kujifunza mbinu lakini si kila mbinu bali zile za ulimwengu wa nuru. Watu wengi wanahangaika na maombi bila kuanza na mbinu. Maombi yanahitajika lakini yana mahali pake. Maombi hutumika kwa ajili ya kutekeleza mbinu ili zifanikiwe. Sasa watu wengi hutumia maombi bila kuwa na mbinu sijui wanatekeleza nini? Ndio maana ukiangalia wakristo wengi ni maskini na wasiomjua Mungu ni matajiri na jambo hili linawasumbua waliokoka kiasi cha kukata tamaa.
Kama utakumbuka mtu mmoja alimwendea Yesu akamuuliza, "Nifanye nini ili niurithi uzima wa milele?" Huyu mtu alikuwa akitafuta kujua ni mbinu gani ingemuwezesha kufanikisha safari yake ya kwenda mbinguni kwani alijua kwenda kanisani haitoshi. Kusoma tu bila kuwa na mbinu za kukusaidia kufaulu mtihani ni bure maana unaweza kushindwa shule. Hujawahi ona mtu anakuambia mimi najitahidi kusoma sana lakini sifaulu. Hivi unadhani tofauti ya wa kwanza na wa mwisho darasani ni nini? Ukijaribu kutazama kwa mapana utagundua ni mbinu.
Jambo la msingi mbinu za mafanikio ni nyingi na hazifanani kwa kila mtu kwa kuwa hutegemea na mazingira na aina ya mtu. Kila mtu duniani ana mpango wake wa maisha usiofanana na mtu yeyoye duniani. Hivyo basi kuiga mbinu za mtu huweza kukukwamisha kimaendeleo. Kwa sababu ya wengi kuwa wavivu wa kusoma biblia na kufikiri huishia katika kuiga walichofanya wengine wakidhani watafanikiwa. Kuna msemo, usemao ni mpumbavu tu anayeweza kutumia njia ile ile akiamini itampa matokeo tofauti.
Mungu ametamani kutupitisha kwenye shule ya namna hii kwa sababu amesema wazi kuwa mawazo anayotuwazia ni mema kutupa tumaini siku zetu za mwisho. Hivyo basi ni rai yangu mpendwa unayefuatana nami kwa njia ya Roho Mtakatifu akupe kuelewa hili ili usikae gizani kamwe maana ndio mpango wa Mungu juu yako.
Barikiwa                                                                                                                                                                 Na Henry Nicholaus

IJUE SADAKA KWA UNDANI WAKE
Sadaka ni kitu chochote kinachoweza kutolewa na mtu kama sadaka. Iwe ni kazi za ajira, mashamba, biashara nk. Ili sadaka iwe sadaka lazima ifanyike kuwa sadaka. Kwa mfano: Noti ya elfu kumi inabaki kuwa noti ya elfu kumi kabla haijafanyika sadaka. Ili elfu kumi iwe sadaka lazima, ni lazima iwe sadaka kwa mtoaji, ili ifanyike sadaka kwa mpokeaji. Kinachofanya elfu kumi iwe sadaka si fedha yenyewe ila ni moyo wa mtu anayeitoa. Kutoka 25:1-2 “Bwana akanena na Musa, akamwambia, waambie wana wa Israeli kwamba wanitwalie sadaka, kila mtu ambaye moyo wake wampa kupenda mtatwaa kwake sadaka yangu,” Sasa utanielewa kuwa uhalali wa fedha kuwa sadaka watoka moyoni na huo humfanya Mungu aipokee.
Kinachofanya gari liwe gari, ni ule mfumo wa utendaji kazi wa injini yake. Kama vile injini ya ndege ndio inayofanya ndege iwe ndege. Pamoja na kwamba kuna aina tofauti za magari kama Toyota, Nissan, Ford, Mistubishi nk; bado yote ni lazima yawe na injini zenye mfumo wa utendaji kazi wa gari kabla hazijawekwa vitu vinavyoitofautisha aina ya hayo magari. Kumbuka sadaka inafanya kazi kama gari. Haijalishi anayeendesha ni mchungaji au ni mwizi bado itafanya kazi kama gari.
Utendaji kazi wa sadaka unafanya kazi kwa kufanana, bila kujali ya kwamba ni Mungu anayepokea au ni miungu inayopokea. Kwa mfano sadaka inamuunganisha mtoa sadaka na Mungu aliyepokea au ni miungu iliyopokea. Soma Zab 106:19,28 na Hes 25:1-3. Pia biblia inatuambia kuwa sadaka inaweza kutumika kumfunga mtu kwa ajili ya kiapo kwa Mungu aliyeipokea au kwa miungu iliyo ipokea Yos 2:12-13,17-21 na Eze 21:21-23.
Tena biblia inatuambia kuwa sadaka inauwezo wa kutengeneza mahusiano ya kimaagano, kati ya mtoa sadaka na Mungu aliyeipokea sadaka yake, au na miungu iliyopokea sadaka yake Zab 50:5. Muunganiko huu haumgusi tu yule aliyetoa sadaka bali nguvu iliyomo ndani ya sadaka aliyoitoa. Inatoa nafasi na uhalali wa kugusa watu wengi zaidi yake hata kugusa kizazi zaidi ya kimoja.
Biblia inatupa mifano ya familia kadhaa ambazo hali zake za kimaisha, kiroho na kimwili zimetengenezwa na utoaji wa sadaka kwa mmoja wa familia zao. Hebu tazama mfano huu: Ibrahimu aliitoa sadaka hii ya fungu la kumi kwa mara ya kwanza, kama tusomavyo katika kitabu cha Mwanzo 14:18-20. Sadaka hii si tu kwamba ilimgusa Ibrahimu na kumwezesha kuwa tajiri bali pia iligusa Lawi na uzao wake kizazi cha nne.
Maisha yako yaweza yakawa yamejengwa juu ya utoaji sadaka wa uzao wako uliokutangulia kuzaliwa katika vizazi vilivyopita. Haya tunayaona katika Zab 50:5 ambapo Mungu akasema, "nikusanyieni wacha Mungu wangu, waliofanya agano nami kwa dhabihu" Hii ni kwa sababu si kwamba watu walitoa wao lakini walitoa kupitia Ibrahimu ambaye ni baba yao. Hivyo kwa kutoa kwake sadaka ya agano kuliwagusa mpaka wao.
Kufuatana na Mwanzo 15:13-16 Mungu alimtaarifu Ibrahimu ya kwamba sadaka yake hiyo, iliyosababisha wakafunga agano pamoja itagusa maisha ya uzao wake miaka mia nne baadaye! Tunaona jambo hili likitokea katika Kut 2:23-24 wakati wana wa Israeli wakimlilia Mungu awatoe toka katika kongwa la utumwa huko Misri. Biblia inasema, "Mungu akasikia kuugua kwao, Mungu akakumbuka agano lake alilofanya na Ibrahimu.."
Sasa utaona kuwa kuanzia sasa utoaji wako wa sadaka ukibadilika kwa sababu umepata kozi mpya juu ya sadaka. Hii inatupa sisi kujua ya kuwa bado kuna hazina kubwa ya maarifa ambayo mimi na wewe twapaswa kuyajua kuwapo duniani ili kuishi kwetu kuwe na faida kwetu sisi leo, kwa wengine tunaoishi nao na hata vizazi vijavyo. Lakini yanategemea kama tutajiegemesha katika kufahamu tunachotakiwa kujua.
Barikiwa                                                                                                                                                                  Na Henry Nicholaus

JE WAJUA KUWA DHAMBI HULETA ADHABU, UADUI, UHARIBIFU NA KUFUNGWA KWA MILANGO YA KI-MUNGU KWA WALIOISHIRIKI
Watu wengi tunatenda dhambi huku tukifikiri tutatubu halafu basi. Leo Mungu ameleta somo hili kwa watu aina hii ili wajue kutenda dhambi kuna gharama kubwa kuliko ile tunayofikiri. Na ndio maana kichwa cha somo kinasema, "Dhambi huleta uadui, adhabu, uharibifu na kufungwa milango ya ki- Mungu kwa wanaoishiriki". Hii ni somo muhimu sana mpendwa naomba ufuatilie nami ueweze kuelewa juu ya jambo hili.
Kwanza nataka utambue kuwa tunachambua kilichopo ndani ya 'sheria ya dhambi na mauti'. Sitaweza kuchambua tena sheria ya dhambi na mauti ni nini, kama huijui ni vema ukatafuta somo moja wapo katika kurasa hii katika hii blog liitwalo "KWA NINI TUNAFANYA MAOMBI YA TOBA" .Hapo utaelewa juu ya sheria ya dhambi na mauti kisha rudi uendelee kusoma somo hili.
"Bwana akamwambia Musa, Haya! shuka; kwa maana watu wako uliowatoa katika nchi ya Misri wamejiharibu nafsi za, wamepotoka upesi kuiacha ile njia niliyowaamuru, wajifanyizia ndama ya kuyeyusha, wakaiabudu na kuitolea dhabihu, wakasema, Hiyo ndiyo miungu yako, Ee, Israeli, iliyokutoa katika nchi ya Misri. Tena Bwana akamwambia Musa, Mimi nimewaona watu hawa na tazama ni watu wenye shingo ngumu, basi niache, ili hasira zangu ziwake juu yao, niwaangamize; nami nitakufanya wewe uwe taifa kuu." Kut 32:7-10
Anagalia maneno yafuatayo na maana zake kama yalivyotumika katika kifungu hapo juu cha maandiko. Neno 'Basi niache ili hasira yangu' hili lilikuwa linaonyesha kuwa Mungu alitaka kuwapa adhabu juu ya dhambi ya kuabudu miungu waliofanya. Pia neno 'Niwaangamize' limeonyesha juu ya uharibifu utakaotokea juu yao. Vilevile neno 'Nami nitakufanya wewe kuwa taifa kubwa' inaonyesha kufungwa kwa milango ya ki-Mungu katika maisha yao.
Na ukisoma Kut 33:2 unaona kuwa Mungu anamwambia Musa licha ya kwamba amebadili msimamo wa kuangamiza Israeli lakini hataendelea nao katika safari bali atawapa malaika ambaye atawaongoza katika safari. Hii inamaanisha kuna kitu kilisababisha 'uadui' kuinuka kati ya watu na Mungu. Na uadui huu uliinuka kwa sababu ya dhambi. Na pia unaweza kunielewa vizuri kama ukisoma Efe 2:13-16, Paulo ametumia maneno yasemayo damu ya Yesu imetumika kuondoa kiambaza kwa tafsiri ya kiambaza ni uadui. Kwa hiyo kama angetumia maneno ya kawaida angesema, Damu ya Yesu ili tumika kuondoa uadui.
Kwa hiyo nimekuonyesha dhambi inaachilia nini pale unapoitenda, angalia kwa karibu maneno yaliokolezwa wino kama hujanielewa. Kwa dhambi ya kuabudu miungu Musa alifanya toba 5 za aina tofauti ili kuwasaidia wana wa Israeli warejee hali yao ya kawaida ya kimwili na kiroho. Hii ina maanisha nini tunaweza kufanya dhambi halafu ikatuadhiri sana hata kama una elimu juu ya sheria ya dhambi ya mauti usifanye makusudi jifunze kuzuia kumbuka aina ya toba alizofanya Musa zilimgharimu muda sana, kwa kuwa sio jambo rahisi.
Nikukumbushe kuwa kujirusha ndani ya shimo ni rahisi kuliko kutoka ndani ya shimo. Hivyo ni vyema ukaomba Mungu akusaidie uepuke kufanya dhambi. Mungu anaposema kuwa anakuwazia yalio mema ndio maana yake ni pamoja na kujua ukweli juu ya mambo mbalimbali kama huu aliokupa leo. Toba ina mambo mengi haya uliojifunza leo si ukomo kwa kuwa hatufiki ukomo wa kujifunza neno la Mungu duniani twahitajika kujifunza kila iitwapo leo.
Barikiwa sana                                                                                                                                                        Na Henry Nicholaus 


No comments:

Post a Comment